Kisa Klopp, Guardiola atoa machozi 

Muktasari:

  • Guardiola aliiongoza City kutwaa ubingwa wa sita ndani ya misimu saba jana baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya West Ham ambapo timu yake ilifikisha pointi 91 mbili mbele ya Arsenal iliyomaliza nafasi ya pili.

Manachester, England. Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola jana alimwaga machozi baada ya kuulizwa swali kuhusu kuondoka kwa meneja wa Liverpool, Jurgen Klopp.

Klopp jana aliiongoza Liverpool kwenye mchezo wa mwisho na kuachana na timu hiyo, akiwa anasema kuwa anataka kwenda kupumzika.

Guardiola aliiongoza City kutwaa ubingwa wa sita ndani ya misimu saba jana baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya West Ham ambapo timu yake ilifikisha pointi 91 mbili mbele ya Arsenal iliyomaliza nafasi ya pili.

"Nitammisi sana, Jurgen amekuwa mtu muhimu sana kwenye maisha yangu ya soka, amenifanya niwe kwenye levo nyingine kwenye maisha yangu.

"Nafikiri tunaheshimiana kila siku na ni mtu wangu wa karibu sana, naona bado anaweza kurudi, nataka kumshukuru sana kwa maneno yake," alisema Guardiola huku akifuta machozi.

Ijumaa iliyopita, Klopp alisema Guardiola ndiye kocha bora zaidi duniani kwa sasa jambo ambalo waandishi walimuuliza Pep anajisikiaje baada ya kauli hiyo.

Klopp ambaye ameshatwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu ya England na Klabu Bingwa Dunia amemaliza msimu wa mwisho timu yake ikishika nafasi ya tatu pointi tisa nyuma ya vinara Manchester City.