Kisa Liverpool, PSG yabanwa ikitaka kuahirishwa mechi Ufaransa
Muktasari:
- Katika msimamo wa ligi, PSG inaongoza kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Lens, hali inayofanya mechi hiyo kuwa na uzito mkubwa katika mbio za ubingwa.
PSG imejikuta ikiingia kwenye mvutano na wapinzani wao wa karibu, Lens baada ya kuwasilisha ombi la kutaka kuahirishwa kwa mechi yao ya Ligi Kuu Ufaransa ‘Ligue 1’ ili kujipatia maandalizi bora kabla ya kukutana na Liverpool katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
PSG, ambao ni mabingwa watetezi wa Ulaya, wanatarajiwa kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Liverpool, Aprili 8, 2026 jijini Paris, kabla ya kurejeana katika dimba la Anfield, Aprili 14, 2026.
Katikati ya ratiba hiyo ngumu, PSG watakuwa na mechi ya ligi dhidi ya Lens iliyopangwa kufanyika Aprili 11, 2026 jambo lililowasukuma kuomba mechi hiyo isogezwe mbele ili kuwapa muda zaidi wa kupumzika na kujiandaa.
Hata hivyo, ombi hilo halikupokelewa vizuri na Lens, ambao wamelikataa na kuliacha suala hilo mikononi mwa Bodi ya Ligi Kuu Ufaransa (LFP), kwa ajili ya uamuzi wa mwisho.
Inataarifiwa kuwa Lens walikuwa tayari kulifikiria ombi hilo endapo lingekuwa na manufaa kwao pia, lakini hali hiyo haikuonekana kuwepo.
Kwa mujibu wa taarifa, PSG walipendekeza mechi hiyo isogezwe hadi Mei, lakini Lens wamepinga vikali wakieleza kuwa kufanya hivyo kungewaweka kwenye ratiba mbaya wakikaa bila mechi kwa takribani wiki mbili, kisha kulazimika kucheza mechi tatu ndani ya wiki moja, hali ambayo wanaona haiendani na uwezo wao wa kifedha na kiushindani.
Kocha wa Lens, Pierre Sage, ameeleza kuwa klabu yake haikubaliani na wazo la kubadilisha ratiba kwa maslahi ya timu nyingine.
Amekiri kuwa kupumzika kunaweza kusaidia timu kufanya vizuri, lakini pia akasisitiza umuhimu wa kuheshimu ratiba na ushindani wa haki.
Mvutano huu umeibua mjadala mpana kuhusu kipaumbele kinachopewa michuano ya Ulaya ikilinganishwa na ligi za ndani.
Lens, kupitia taarifa rasmi, wameeleza wasiwasi wao kuwa ligi ya Ufaransa inaonekana kupoteza thamani yake kwa kupewa nafasi ya pili nyuma ya mashindano ya kimataifa, jambo walilodai si la haki kwa klabu nyingine.
Wamesema kuwa kubadilishwa kwa ratiba hiyo kungeonyesha kuwa klabu ndogo zinapaswa kujinyenyekeza kwa maslahi ya klabu kubwa, hali ambayo wanaiona kuwa inahatarisha misingi ya ushindani sawa katika soka la Ufaransa.
Kwa upande wa PSG, hili si tukio la kwanza kupewa nafuu ya ratiba.
Wiki iliyopita, walifanikiwa kuahirisha mechi yao dhidi ya Nantes kabla ya kukutana na Chelsea katika hatua ya 16 bora ya Ulaya, ambapo waliibuka na ushindi mkubwa wa jumla wa mabao 8-2. Hali hiyo imeongeza hoja ya Lens kwamba PSG wanafaidika zaidi na maamuzi ya ratiba.
Uamuzi wa mwisho sasa unasubiriwa kutoka katika shirikisho la Soka la Ufaransa huku macho ya wadau wa soka yakielekezwa kuona iwapo mamlaka hiyo itaegemea upande wa PSG kwa maslahi ya uwakilishi wa Ufaransa barani Ulaya, au itasimamia misingi ya ushindani wa ndani kama inavyotetewa na Lens.
Katika msimamo wa ligi, PSG wanaongoza kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Lens, hali inayofanya mechi hiyo kuwa na uzito mkubwa katika mbio za ubingwa.