Kocha mpya Simba ni huyu...

Muktasari:

  • BILIONEA wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji ameondoka nchini juzi Jumapili kwenda Dubai, huku nyuma akiweka mazingira mazuri kwa mabosi wa klabu hiyo katika kukisuka kikosi cha timu hiyo, lakini utamu zaidi ni ishu ya kocha mkuu mpya ambapo kwa sasa anakuja Mslovakia.

BILIONEA wa Simba, Mohammed ‘Mo’ Dewji ameondoka nchini juzi Jumapili kwenda Dubai, huku nyuma akiweka mazingira mazuri kwa mabosi wa klabu hiyo katika kukisuka kikosi cha timu hiyo, lakini utamu zaidi ni ishu ya kocha mkuu mpya ambapo kwa sasa anakuja Mslovakia.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema Mo Dewji amewaachia mkwanja mrefu viongozi wa timu hiyo kuhakikisha wanakamilisha dili la wachezaji wapya na kocha wa kuziba nafasi ya Pablo Franco, huku ikipenyezwa kuwa Josef Vukusic ndiye anayepewa nafasi kubwa.

Vukusic aliyewahi kuzinoa Polokwane na Amazulu za Afrika Kusini ni kati ya majina mawili ya mwisho yaliyokuwa kwenye mchujo wa kusaka kocha mkuu mpya na uzoefu wake kwa soka la Afrika na dau lake, vimeivutia Simba.

Amazulu ndio klabu anayoenda kujiunga nayo kiungo wa Simba, Rally Bwalya ambaye usiku wa jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa alikuwa akiagwa rasmi katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC. Klabu hiyo pia ilihusishwa kumtaka Pablo hata kabla hajatimuliwa Msimbazi.

Mwanaspoti limepenyezewa kuwa raia huyo wa Slovakia aliyeachana na FC Kosice, Mei mwaka huu ndiye atakayepewa mikoba ya Pablo, ingawa uamuzi wa mwisho unategemea kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa Simba itakayokutana kupitisha jina moja kati ya mawili yaliyopo.

Jina la kocha wa pili anayechuana na Vukusic halijapatikana, licha ya juhudi za Mwanaspoti kupambana kulinasa, ikielezwa kuwa anayelifahamu ni ofisa mtendaji mkuu, Barbara Gonzalez pekee na yeye ndiye atakayewasilisha mezani kwa wajumbe kufanya uamuzi ya mwisho.

Chanzo hicho kilieleza kuwa Vukusic ni kati ya makocha wa mwisho wa mchujo kufanyiwa usaili na Barbara na anaonekana kuivutia Simba kwa wasifu na upatikanaji wake.

Inaelezwa hana timu kwa sasa, lakini pia uzoefu wake kwa soka la Afrika, kwani inadaiwa Pablo enzi zake alikuwa akijitetea pale anapobanwa juu ya kutofahamu vyema soka la Afrika, jambo ambalo mabosi wa Simba kwa sasa hawataki kulisikia.

“Vukusic alifanyiwa usaili na alifanya vizuri kama vile ambavyo ilikuwa inahitajika ikiwemo kueleza kuwa anaweza kurudisha heshima ya Simba iliyopotea msimu huu katika Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho ASFC na Ligi ya Mabingwa Afrika iliyoondolewa hatua za mtoano,” kilisema chanzo hicho.

Inaelezwa mbali na wasifu na uzoefu, lakini kocha huyo alimtwangia simu Pablo kumuulizia maisha na mazingira ya Simba na kutaka kujua aina ya wachezaji waliopo na taratibu nyingine ambazo zingemsaidia kuijua kwa undani timu hiyo kabla ya kuja kuanza kasi rasmi.

“Tayari jamaa amempigia simu na kuzungumza na Pablo ili kujua mazingira ya Tanzania na ishu za kiufundi na mengineyo. Bahati nzuri alimjibu vizuri na kumuelekeza maisha yote ndani ya Simba, ni kama Vukusic alikuwa akihitaji pamoja na mengine ambayo hakuwa anafahamu na mwisho wa yote alimtakia kila la heri kwenye kazi yake mpya,” kilisema chanzo hicho.

Pablo alipotafutwa na Mwanaspoti japo hakupenda kulifafanua, alikiri ni kweli alipigiwa simu na Vukusic zaidi ya mara moja kutaka kufahamu taarifa za Simba.

“Ni kweli amewasiliana nami zaidi ya mara moja, ila tulichozungumza ni mambo yetu,” alisema Pablo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alipoulizwa, alisema mchakato wa kumpata kocha bado haujafikia mwisho ila wapo pazuri.

“Bado hutujafika mwisho, ila tukikamilisha tutaliweka wazi na kila mtu atajua msimu ujao tutaanza na kocha gani. Ndio maana hata usajili suala la kambi ya maandalizi ya msimu (pre season) limesimama,” alisema Try Again.


WASIFU WA VUKUSIC

Vukusic alizaliwa Agosti 3, 1964 na sasa ana umri wa miaka 57, eneo la Kosice na alianza kucheza soka la vijana 1975-1983, katika timu ya VSZ Kosice baada ya hapo akacheza soka la ushindani timu mbili 1983-1992 alicheza VSZ Kosice baadaye alijiunga na VFL Rheinbach kabla ya kuanza kuwa kocha.

Maisha ya ukocha alianza 1994-95 akiwa kocha mchezaji wa Kosice kisha akatua VFL Rheinbach baada ya hapo 2000-03 alitua Steel Trans kisha akafundisha msimu mmoja Ruzomberok 2003-04 zote za Slovakia.

Kocha huyo mwenye leseni ya Uefa Pro 2004 alifundisha Spartak Trnava kisha 2005-09 alifundisha timu ya vijana ya taifa lake Slovakia U-2 kama kocha msaidizi kisha akatua Afrika 2010-12 kwa kuinoa Cape Town ya Sauzi kabla ya kujiunga na Nitra (2012-13) na 2013-14 alitua Ruzomberok.

2014 aklirudi tena Afrika kuinoa Al-Ahly ya Libya kabla ya kwenda VSS Kosice na 2016 alitua Shakhter Karagandy ya Kazakhstan na 2017 alifundisha Spartaks Jurmala ya Slovakia na kubeba nao ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na 2018-19 alitua tena Sauzi kuinoa Polokwane City na msimu mmoja baadaye alihamia AmaZulu na msimu uliopita alijiunga na FC Kosice anayoelekea kumalizana nayo mkataba.