Majonzi yatanda bondia aliyeuawa na gari

Muktasari:
- Bondia bingwa wa zamani wa Dunia wa Super Middle na Light Heavy, Graciano Rocchigiani wa Ujerumani aliyecheza mapambano 48 kushinda 41, yakiwemo 19 kwa KO, kushindwa mara sita na sare moja, amefariki Dunia akiwa na miaka 54 kwa kugongwa na gari akifanya mazoezi ya jioni nchini Italia.
Milan, Italia. Bondia bingwa wa zamani wa Dunia uzani wa Super-middle na Light-heavy, Graciano Rocchigiani raia wa Ujerumani, amefariki Dunia baada ya kugongwa na gari Kusini wa Italia hapo jana.
Rocchigiani ambaye baba yake ni Mtaliano na mama Mjerumani, amefariki Dunia akiwa na miaka 54, ambapo aligongwa na gari wakati akifanya mazozi ya jioni ya kutembea.
Bondia huyo alipata kutwaa Ubingwa wa Dunia unaotambuliwa na IBF uzani wa Super Middle, mwaka 1988 na 1989 kabla ya kutwaa ubingwa unaotambuliwa na WBC uzani wa Light Heavy mwaka 1998 alipomshinda Michael Nunn.
Moja ya mambo ya kukumbukwa kwa Rocchigiani, katika upiganaji wake ni kucheza mapambano yake yote 48 ya kulipwa nchini Ujerumani na alikuwa bondia wa tatu wa nchi hiyo kutwaa ubingwa wa Dunia akitanguliwa na Max Schmeling na Eckhard Dagge.
Mwaka 2003 Rocchigiani alicheza pambano lake la mwisho la ngumi za kulipwa akiusaka ubingwa wa Dunia wa WBC uzani wa Light Heavy, lakini alishindwa.
Maelfu ya mabondia na wadau wa mchezo wa ngumi wameanza kutuma salamu za rambi rambi na Meya wa mji wa Berlin, Michael Mueller, amesema wameguwa na msiba huo na kukiri Taifa la Ujerumani limepoteza shujaa mbaye mchango wake ulikuwa bado unahitajika.