Mambo matano dakika 90 Euro 2024

Muktasari:

  • Ujerumani ilianza vyema michuano ya Kombe la Euro 2024 baada ya kuifunga Scotland mabao 5-0 katika mechi ya ufunguzi.

Munich, Ujerumani. Michuano ya Kombe la Euro ilianza jana nchini Ujerumani kwa wenyeji kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Scotland kwenye Uwanja wa Munich Arena.

Huu ulikuwa mchezo mkali wenye msisimko wa hali ya juu, huku timu zote zikionyesha kiwango kizuri uwanjani.

Mchezo huo wa ufunguzi ulionyesha kuwa Ujerumani imejipanga vyema kuhakikisha kuwa inataka kufanya vizuri kwenye michuano ya mwaka huu ili kutafuta ubingwa wake wa nne ikiwe kwenye aridhi ya nyumbani.

Kuna mambo kadhaa yalitokea kwenye mchezo huo wa ufunguzi ambayo mashabiki wa soka duniani kote wanataka kuyafahamu.


Mabao matano, wachezaji watano

Ujerumani imeonyesha kuwa inataka kuchukua ubingwa wa msimu huu baada kuanza kwa ushindi wa mabao 5-1 huku kila bao likifungwa na mchezaji mmoja, ambapo wafungaji walikuwa Florian Wirtz, Jamal Musiala, Kai Havertz, Niclas Fullkrug na Emre Can.


Hakuna shuti lolote

Jambo lingine lililotokea la kushtua ni kwamba wageni hao hawakupiga shuti lolote lililolenga lango, wakiwa wamepiga moja tu nje ya lango la Ujerumani.

Wakati wenyewe wakifanya hivyo, wenyeji walipiga mashuti 10 nje ya lango na 9 yaliyolenga lango wakionyesha kuwa waliutawala mchezo huo kwa sehemu kubwa.


Kona 5-0

Ujerumani ilipiga kona tano kwenye mchezo huo, lakini wageni Scotland hawakupiga kona yoyote ndani ya dakika zote tisini.


Bao la kwanza la kujifunga

Beki wa Ujerumani, Antonio Rudiger ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kujifunga kwenye michuano ya Euro msimu huu, baada ya kuumalizia mpira wavuni kwa kichwa wakati akijaribu kuokoa shambulizi la Scotland.


Kadi ya kwanza nyekundu

Beki wa Scotland Ryan Porteous, ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kupewa kadi nyekundu baada ya kumchezea madhambi kiungo wa Ujerumani Ilkay Gundogan wakati akielekea kufunga.


Mechi za leo

Michuano ya Euro inaendelea leo wakati Croatia itakapoingia uwanjani kuvaana na Hispania saa moja usiku, huku Italia ikicheza na Albania, Poland na Uholanzi, Hungary na Switzerland.