Manara apunguziwa adhabu, ajibu mapigo

KAMATI ya rufaa ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imempunguzia adhabu msemaji wa Yanga, Haji Manara.

Awali kamati ya maadili ya TFF, ilimfungia msemaji huyo kutojihusisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi kwa miaka miwili na faini ya Sh20 milioni kwa kosa la kumtolea maneno yasiyofaa Rais wa TFF, Wallace Karia katika mechi ya fainali ya kombe la Azam iliyopigwa Jijini Arusha.

Manara alikutwa na hatia hiyo ya kumtishia na kumdhalilisha Karia siku ya Jumamosi Julai 2, 2022 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha wakati wa mechi ya fainali kati ya Yanga dhidi ya Coastal Union.

Kupitia kamati ya rufaa ya maadili ya TFF, Manara amepunguziwa adhabu yake hivyo atatakiwa kulipa Sh10 milioni badala ya kiwango cha awali, atatakiwa kulipa kiasi hicho ndani ya siku 30 huku muda wa kutumikia adhabu ukiwa pale pale.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, ni kama Manara amejibu mapigo ya hukumu hiyo kwa kuandika,"Alfajiri ya leo nilimsindikiza binti yangu mkubwa kurejea Istambul Uturuki,ambako anaendelea na masomo yake ya Shahada ya kwanza nchini humo, akiwa katika mwaka wake wa pili wa masomo.

"Kwangu hilo ndio muhimu kupita haya mengine ya mapito, hususani yanayojiri kila usiku Mkubwa. Watoto wa maskini mtaji wao mkuu ni elimu, ndicho kitu tulichoamrishwa kuwekeza kwao, ukiwekeza katika eneo hilo, kinachobaki ni kumuomba Mungu tu,"

"Ndio, yaliyotangazwa jana na Wafalme juu yangu, ni sehemu ya changamoto zetu za kidunia na niliyatarajia pasi na shaka. Ndugu zangu jamaa, marafiki na Wananchi wenzangu msifadhaike hata tone na hizi hukumu dhidi yangu, haki haijawahi kushindwa milele, ni suala la muda tu."