Mapro wanavyoinogesha Ligi Kuu ya Wanawake (WPL)

Dar es Salaam. Soka la wanawake kwa sasa ni kama ‘lulu’ na ile dhana ya ukatili wa kijinsia kwa jamii inapomuona ‘binti’ akicheza soka imeanza kutoweka.

Mabinti wanatumia fursa ya vipaji vyao kuingiza kipato na kuhudumia familia zao, kujiajiri na wengine kufanya mambo mengine ya maendeleo kutokana na kipato wanachopata kupitia vipaji vyao vya soka.

Mmoja wa wachezaji maarufu nchini anasema miaka ya nyuma baadhi ya jamii iliwachukulia kama wanawake wanaocheza soka wanafanya uhuni.

“Nakumbuka wakati naanza kucheza, niliambiwa hakuna mafanikio kwenye soka la wanawake, familia ilinitaka nisome tu, ilifikia hatua baada ya vipindi vya darasani nikienda mazoezini nyumbani hakukaliki, napewa adhabu.

“Wazazi wangu, hasa baba hakuamini kuhusu mtoto wa kike kucheza mpira wa miguu, hata hivyo sikukata tamaa, nilipoitwa kwenye timu ya taifa ndipo wakashtuka.

“Sasa nimesajiliwa na klabu ya Simba, nalipwa vizuri na hata familia yangu inakula matunda ya kipaji changu, nalipwa mshahara na wadogo zangu nawasomesha kwa pesa ya mpira,” anasema mchezaji huyo.

Hamasa kwenye soka la wanawake imeanza kuonekana, mafanikio ya timu za wanawake ni uthibitisho ikiwamo ya Taifa ya vijana (U-17), Serengeti Girls, ilipofuzu kushiriki mashindano ya Dunia, ikiwa ni timu ya kwanza ya soka nchini iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuiwakilisha nchi kwenye Kombe la Dunia.

Mbali na timu za Taifa, Tanzania ilifungua milango kwa nyota wa kigeni kujiunga na klabu za Ligi Kuu ya Wanawake bila mipaka, fursa ambayo Chama cha Soka cha Wanawake (TWFA) kinasema imeonyesha mwanga kwenye ligi hiyo.

Hata hivyo, sasa kanuni zinataka kila klabu kusajili nyota 12 na wote wanaruhusiwa kuwa kwenye kikosi kinachocheza, fursa ambayo Yanga Princess wameitumia ipasavyo kwa kuwa na nyota wote wa kigeni.

Hivi karibuni, kocha Sebastian Nkoma aliwaanzisha maproo wake tisa kwenye dabi na Simba Queens, mechi ambayo ilikuwa gumzo kutokana na ubora, usajili na rekodi za timu hizo.

Kikosi cha mapro wa Yanga kinaongozwa na Tessy Biahwo (Nigeria), Salifu Safiatu (Ghana), Wingate Kaari (Kenya), Mary Saiki (Nigeria) Blessing Nkor (Nigeria), Aniella Uwimana (Burundi), Prescious Onyinyechi (Nigeria), Pauline Kathuruh (Kenya), Foscah Kanenge (Kenya), Marry Mushiya (Congo DR), Nadege Atanhloueto (Benin) na Wogu Success (Nigeria).

Kocha Nkoma anasema uwepo wa nyota wa kigeni nchini umeongeza ushindani kwenye ligi hiyo ambayo imeanza kufuatiliwa kwa karibu na wadau wengi wa soka.


Simba Queens yenyewe ina maproo 11 ambao ni Pambani Kuzoya Falonne (Congo), Barakat Olaiya (Nigeria), Joelle Bukuru (Burundi), Asha Djafari (Burundi), Vivian Corazone (Kenya), Topister Situma (Kenya), Philomena Abakah (Ghana), S’arrive Badiambila (Congo), Daniela Ngoyi (Congo) na Carolyne Rufa (Kenya).


Timu nyingine zenye maproo ni Alliance Girls ambao ni Anita Adongo Agunda (Kenya), Florida Omusanga (Kenya), Adelaide Nimfasha (Burundi) na Akinyi Otieno Damas (Kenya).


Fountain Gate Princes ina nyota wa kigeni wengi kutoka Kenya ambao ni Peris Oside, Myline Awuor, Inviolata Mukoshi, Amakobe Esther Meya, Chebeti Monicah Odata na Mrundi, Niyonkuru Sandrine.

Kwenye kikosi cha Ruvuma Queens kuna maproo wawili wa Burundi, Munezero Umurundi na Bukuru Rachele sanjari na Mzambia, Dorothy Mukatasha, wakati kwenye kikosi cha The Tiger Queens mchezaji wao wa kimataifa ni Charlotte Irankunda (Burundi)

Timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu ya wanawake ni Amani Queens, Ciassia Queens, Baobab Queens na JKT Queens.

“Ujio wa wageni maana yake Ligi yetu ni kubwa, imeimarika na ina ubora, TWFA tukilinganisha tulipotoka na tulipo, soka la wanawake nchini linaedelea kupiga hatua,’ anasema Somoe Ng’itu, katibu mkuu wa TWFA.

Anasema wachezaji wakigeni wameongeza hamasa kwenye Ligi ya wanawake na nyota wazawa sasa wanapaswa kupambana ili kuhakikisha wanapata nafasi ya kuwa kwenye vikosi vya kwanza vya timu zao.

“Hata hivyo, kwa maslahi mapana ya timu yetu ya taifa, kwa misimu ijayo tutafikiria kubadili kanuni ya usajili wa wachezaji wa kigeni, ili kuisaidia timu ya taifa,” anasema.

Alex Alumirah kocha wa Fountain gate anasema Ligi inapokuwa na wachezaji wa kigeni, kwanza inajitangaza nje ya mipaka yake kupitia nyota hao.

“Pia inaongeza ushindani, na habari njema ni kwamba soka la wanawake huko duniani linakuwa kwa kasi, hivyo mnapokuwa na Ligi bora na soka lenu linakuwa,” anasema.


Jamii yabadili mtazamo

Hivi karibuni, Somoe akiwa miongoni mwa watoa mada katika semina iliyoandaliwa na TWFA kwa kushirikiana na Taasisi ya Global Peace Tanzania (GPF Tz) iliyokuwa na maazimio ya kutokomeza vitendo vya ukatili kwenye michezo hususani katika soka la wanawake, alieleza namna ambavyo ukatili wa kisaikolojia na kijinsia ulivyokuwa kikwazo kwa wanawake.

Semina hiyo iliyofadhiliwa na Woman Fund Tanzania Trust , ilionyesha matokeo ya ukatili wa kijinsia michezoni, hususani katika soka la wanake, baada ya GPF Tanzania kufanya utafiti katika miji ya Dar es Salaam, Zanzibar na Dodoma kisha kutoa elimu ambayo kw kiasi fulani ilibadili fikra za jamii kubwa kuhusu soka la wanawake.

“Tumeanza kupiga hatua, zile fikra za kutoamini kuna fursa kwenye soka la wanawake zimepungua kwa kiwango kikubwa, sasa jamii, wazazi na walezi wanatambua kuna fursa kubwa ya ajira huku.

“Wachezaji wanasajiliwa wanalipwa ada ya usajili, wanalipwa mishahara kila mwezi, kama ambavyo inafanyika kwa wachezaji wa kiume, wanasoka wanawake wengine wanahudumia familia zao kwa kipato cha mpira,” anasema.

Mkurugenzi wa GPF Tanzania, Martha Nghambi anasema mwamko wa jamii kuanza kuondoa dhana ya ukatili wa kijinsia michezoni hasa kwenye soka la wanawake kunazidi kuongeza fursa kwa vijana wenye vipaji nchini akiishukuru TWFA na Woman Fund Tanzania Trust kusapoti mafunzo ya kutokomeza ukatili wa michezoni hususani kwenye soka la wanawake.

Mwamko huo umeendelea kuzaa matunda, soka la wanawake kilipigiwa hesabu za kuwa miongoni mwa michezo ya kipaumbele iliyotajwa na wizara ya michezo.

Pia, Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ilieleza namna ambavyo Tanzania inaweza kufuzu kushiriki michezo hiyo kupitia timu ya wasichana ya soka, na kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza nchini ya soka kufuzu kushiriki Olimpiki baada ya ‘kaka’ zao U23 kukosa tiketi hiyo mara kadhaa.

Ukiachana na riadha, ngumi, judo na kuogelea ambao wamekuwa wakishiriki Olimpiki, soka la wanawake ni miongoni mwa michezo ambayo inapewa nafasi kubwa ya kufuzu na kufanya vizuri zaidi kimataifa.