Maswali matatu hatima ya Fei Toto

Dar es Salaam. Maswali matatu yameonekana kuzua mijadala baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuitaka Yanga ifikie muafaka na kiungo Feisal Salum ‘Feitoto’ ambaye amegoma kuendelea kuitumikia akidai anataka mkataba uvunje awe huru.

Rais Samia alitoa wito huo katika hafla ya kuipongeza Yanga kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo aliishauri timu hiyo kumaliza suala la kiungo huyo. “Viongozi wa Yanga nina ombi kwenu. Sifurahii kusikia mnakuwa na mizozo na wachezaji na sitaki kusema mengi, nataka niwaambie tu, hii ishu ya Fei Toto, hebu kaimalizeni,” alisema.

"Kalimalizeni ili tuangalie mbele. Haipendezi klabu kubwa kama hii iliyofanya kazi nzuri, mnakuwa na ka ugomvi na katoto. Hebu kamalizeni mwende vizuri. Nitasubiri kupata mrejesho wa hili, siku yoyote mkiwa tayari karibuni nyumbani mje kunipa mrejesho.”

Swali la kwanza linaloibuka baada ya kauli hiyo ya Rais Samia kama Yanga itakuwa tayari kuvunja mkataba wa Feitotoau itaendelea na msimamo wa awali wa kumtaka arejee kundini.

Ikubukwe kuwa baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuamuru kiungo huyo kurejea Yanga, klabu hiyo ilimuandikia Feitoto ikimtaka ajiunge na timu kutumikia mkataba.

Swali la pili ni iwapo Feitoto ataendelea na msimamo wa kuishtaki Yanga katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) au ataachana nayo?

Na la tatu ni iwapo pande hizo zikishindwa kufikia muafaka ni hatua gani ambazo Rais atazichukua kushughulikia suala hilo?

Mchezaji wa zamani Simba na Yanga, Zamoyoni Mogela alisema kauli ya Rais kwa Yanga ni kama mtego na ni mtihani mkubwa kwani Yanga na Feitoto wanatakiwa kukaa chini. "Kauli ya Rais sasa nadhani ndio itafanya wawili hao kwa pamoja wakae chini na jambo hili litamalizika tofauti na ilivyokuwa awali,"alisema Mogela.

Meneja wa zamani wa KMC, Faraji Muya alisema Yanga ina haki ya kimkataba, lakini upande wa nidhamu haitakiwi kuendelea kumng'ang'ania mchezaji ambaye ameshatamka hana furaha kuwa kikosini hivyo ni bora wamalizane.

"Mama ni mtu mwenye huruma na ndio maana amewaomba Yanga wamalizane na Feisal. Wakati sahihi sasa kwa pande hizi mbili kukaa chini na kumaliza haya mambo yanayoendelea," alisema Muya.

Mshambuliaji wa zamani Yanga, Henry Morris, alisema kauli ya Rais ni nzuri kwani Feisal ni kijana hivyo hata kama amekosea inabidi uongozi utumie busara. "Najua viongozi wa Yanga ni watu wenye weledi mkubwa. Wamsamehe Feisal,” alisema Morris