Mayele aipa taji lingine Pyramids, aibuka mfungaji bora
Muktasari:
- Fiston Mayele aliibuka mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2022/2023 ambao pia alifungana na Saido Ntibazonkiza kumaliza akiwa Mfungaji Bora.
Nyota wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele jana Septemba 25, 2025 ameiongoza Pyramids FC kutwaa ubingwa wa Komba la FIFA la African-Asian-Pacific baada ya kufunga mabao yote ya timu yake katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Al Ahli ya Saudi Arabia.
Katika mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa King Abdullah Sports City, Jeddah, Saudi Arabia, Mayele alifunga mabao hayo katika dakika ya 21, 71 na 75 huku lile la Ahli likifungwa na Ivan Toney katika dakika ya 45.
Mabao hayo matatu (hat trick) ya Mayele yamemfanya aibuke Mfungaji Bora wa Mashindano hayo tuzo ambayo pia alichukua miezi mitatu iliyopita katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuifungia Pyramids FC mabao sita.
Jambo la kuvutia zaidi kwa Mayele ni kufunga mabao hayo dhidi ya Al Ahli ambayo ilikuwa na nyota kadhaa waliowahi kutamba katika klabu mbalimbali barani Ulaya miaka ya hivi karibuni.
Toney aliyefunga bao pekee la Al Ahli alikuwa anaitumikia Brentford na wengine na timu walizowahi kuzichezea kwenye mabano ni Eduardo Mendy (Chelsea), Merih Demiral (Atalanta), Franck Kessie (AC Milan), Millot Enzo (Stuttgart), Ryad Mahrez (Man City) na Valentine Atangana (Reims).
Katika mchezo huo, refa Istvan Kovacs kutoka Romania, alionyesha kadi moja tu ambayo ilikuwa ya njano aliyopewa beki wa Pyramids FC, Mohamed Hamdy.
Mayele alijiunga na Pyramids FC mwaka 2023 akitokea Yanga na amefanikiwa kuwa mchezaji tegemeo wa klabu hiyo ya Misri huku pia akipata nafasi ya kuwemo katika kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo.
Baada ya kuipa taji Pyramids FC, Mayele asubuhi ya leo alienda kufanya ziara ya Umrah na kisha akatuma picha katika Ukurasa wake wa Instagram akimshukuru Mungu.