Mdamu afanyiwa upasuaji
Dar es Salaam. Hatimaye aliyekuwa mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Gerald Mathias Mdamu, amefanyiwa upasuaji wa mguu wake wa kulia, ambao ulikumbwa na changamoto ya jibu la kwenye mfupa.
Mdamu alipata ajali mbaya ya kuvunjika miguu Julai 9, mwaka 2021, akiwa na wenzake katika basi la timu ya Polisi Tanzania, likitokea mazoezini Uwanja wa TPC kuelekea kambini,ambapo alifanyiwa upasuaji katika hispital ya taifa ya Muhimbili.
Hivi karibuni, Mwananchi liliibua hali yake kuwa mbaya, alipofanyiwa vipimo (X -ray) katika hospitali ya Muhimbili, akagundulika ana tatizo la jipu katika mfupa.
Kwa mujibu wa mkewe Juliana, alisema mume wake Mdamu alifanyiwa upasuaji jana Ijumaa, hivyo ataendelea na matibabu mengine chini ya madaktari wa hospital hiyo.
"Namshukuru Mungu aliyewapa moyo Watanzania wote waliojiotolea kuhakikisha Mdamu anatibiwa, madaktari hasa nakumbuka jinsi daktari Kennedy Nchimbi alivyompokea kwa mara ya pili, alivyomjenga kiakili kuchukulia ni hali ya kawaida na inatibika, TFF chini ya Rais Karia, makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, Bakari Mwamnyeto na Zawadi Mauya.
"Shukrani za kipekee, nalishukuru gazeti la Mwananchi kwa kuibua hali yake, maana ndio sababu ya Mdamu kupata msaada wa kuchangiwa matibabu yake, familia yangu kwa sasa itakuwa na amani, maana akipona atakuwa anafanya shughuli zake mwenyewe."
Alisema kabla ya kupata msaada wa kuchangiwa pesa za matibabu, walikata tamaa, ila kwa sasa anafurahia na kuona wataendelea na mapambano ya maisha.