Mechi 4, Mosimane afungwa mabao 15

Muktasari:

  • Abha ambayo iliwahi kunolewa na kocha wa zamani wa Simba, Sven Vandenbroeck inashika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia

Kipigo cha mabao 5-0 jana kutoka kwa Al Shabab, kimeifanya timu ya Abha inayonolewa na kocha wa zamani wa Mamelodi Sundowns na Al Ahly, Pitso Mosimane kufikisha idadi ya mabao 15 ya kufungwa katika mechi nne ilizocheza hivi karibuni katika Ligi ya Saudi Arabia.

Timu hiyo ambayo nyota wa Simba, Luis Miquissone aliwahi kuichezea kwa mkopo na pia ikiwahi kunolewa na aliyewahi kuwa kocha wa Simba, Sven Vandebroeck, imeruhusu mabao hayo 15 katika mechi dhidi ya Al Riyadh, Al Nassr, Al Fateh na jana dhidi ya Al Shabab.

Rekodi hiyo mbaya ya safu ya ulinzi ya timu hiyo ya Mosimane ilianzia Machi 30 ilipotoka sare ya bao 1-1 na Al Riyadh na Aprili 2 ikakutana na kipigo kizito cha mabao 8-0 kutoka kwa Al Nassr.

Mchezo unaofuata, Aprili 7, ikapata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Al Fateh na jana ikapoteza kwa mabao 5-0 mbele ya Al Shabab.

Aliyeongoza mauaji ya Abha jana ni nyota wa zamani wa Atletico Madrid, Yannick Ferreira Carrasco aliyepachika mabao mawili kama alivyofanya nyota mwingine wa Al Shabab, Carlos Junior huku bao lingine moja likipachikwa na Mouhamadou Diallo.

Matokeo hayo yameifanya Abha kubakia katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia, ikiwa na pointi 25, moja zaidi ya zile za Al Akhdoud iliyopo katika mstari wa kushuka darasa, nafasi ya 16.

Timu hiyo ya Pitso Mosimane, katika mchezo unaofuata, Aprili 27, itakuwa ugenini kukabiliana na Al Akhdoud ambapo ikipoteza itashuka hadi katika mstari wa kushuka daraja.

Ligi Kuu ya Saudi Arabia imebakiza mizunguko saba kufikia tamati ambapo hadi sasa, Al Hilal inaongoza ikiwa imekusanya pointi 77 ikifuatiwa na Al Nassr yenye pointi 65 wakati Al Ahli inashika nafasi ya tatu na pointi zake 52.