Msuva aweka rekodi Taifa Stars ikihitimisha kwa sare

Muktasari:

  • Licha ya Taifa Stars kushindwa kwenda katika hatua inayofuata ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia, imehitimisha mechi zake kwa heshima huku Simon Msuva akiweka rekodi.


Dar es Salaam. Licha ya Taifa Stars kushindwa kwenda katika hatua inayofuata ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia, imehitimisha mechi zake kwa heshima huku Simon Msuva akiweka rekodi.

Stars ilikuwa Kundi J pamoja na Benin, Madagascar na DR Congo, ambao wamefuzu kwenda hatua ya mtoano kutoka kundi hilo na Msuva ameweza kuzifunga timu zote hizo nyumbani kwao.

Alianza kwa kuifunga DR Congo ugenini katika mechi iliyopigwa nchini humo Septemba 2, mwaka huu na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, kisha akaifunga Benin nyumbani kwao, Oktoba 10, mwaka huu katika ushindi wa bao 1-0 ambapo ilikuwa kama kulipiza baada ya Benin kuifunga Stars 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Bao la jana dhidi ya Madagascar katika matokeo ya 1-1, lilizidi kumfanya Msuva kuwa mchezaji hatari zaidi wa Taifa Stars katika miaka mitatu ya hivi karibuni na kuhitimisha kalamu ya kuzifunga timu zote za kundi J nyumbani kwao.

Mabao hayo matatu ya ugenini, yamemfanya Msuva kuwa kinara wa upachikaji mabao wa Taifa Stars katika hatua ya makundi kufuzu Kombe la Dunia akifuatiwa na Erasto Nyoni, Novatus Dismas, Feisal Salum, wakifunga bao moja kwa kila mmoja wao kwenye hatua hiyo katika mechi moja dhidi ya Madagascar Septemba 7, Stars ikishinda 3-2 kwenye Uwanja wa Mkapa.