Mwanzo wa mwisho wa Samatta Stars

Muktasari:
- Baada ya kuitumikia Taifa Stars kwa miaka 13 ni wazi kwamba Taifa Stars imeanza kujiandaa na maisha bila yeye na hilo linajidhihirisha baada ya jana kutotangazwa kuwemo katika kikosi cha wachezaji 23 ambacho kitacheza dhidi ya Ethiopia
Dar es Salaam. Kuendelea kuwa nje katika kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' kinachojiandaa na mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) mapema mwezi ujao kwa nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta kunaweza kutafsirika kama ishara za kuelekea mwisho wa utegemezi wa nyota huyo wa PAOK ya Ugiriki katika timu ya taifa.
Baada ya kuitumikia Taifa Stars kwa miaka 13 ni wazi kwamba Taifa Stars imeanza kujiandaa na maisha bila yeye na hilo linajidhihirisha baada ya jana kutotangazwa kuwemo katika kikosi cha wachezaji 23 ambacho kitacheza dhidi ya Ethiopia nyumbani, Septemba 4 na kisha ugenini dhidi ya Guinea, Septemba 10.
Kaimu kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco' amesema kuwa Samatta ameachwa ili apate fursa ya kushughulikia masuala yake binafsi.
"Samatta ni nahodha wetu. Kuna masuala anayashughulikia hata Msuva pia kama wangekuwa tayari kwa michezo hiyo basi nisingesita kuwajumuisha kikosini lakini pia muda ni mchache sana,"
Licha ya kocha Hemed Suleiman 'Morocco' kufafanua kwamba Samatta hajaitwa kikosini kwa sababu za kiufundi, kuna sababu mbili ambazo zinaonyesha utegemezi wa nyota huyo wa zamani wa Aston Villa na KRC Genk unaanza kufifia.
Sababu ya kwanza ni yeye mwenyewe kuonekana kutokuwa tayari kuitumikia Taifa Stars na hilo linathibitishwa na barua aliyoandika ya kuomba kustaafu kwenda Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), baada ya kumalizika kwa fainali za Afcon mwaka huu huko Morocco.
“Kuna kuchoka na umri pia unaenda ni lazima nipate wakati wa kupumzika, mashabiki wamenilea wengi wao wameniona tangu nikiwa kijana mdogo kwa kiasi kikubwa mafanikio niliyoyapata wao wamechangia,” alisema Samatta katika mahojiano yake na gazeti la Mwanaspoti baada ya uamuzi huo wa kustaafu Stars.
Sababu ya pili ni kutokuwa katika kiwango bora katika miaka ya hivi karibuni kuanzia katika timu ya taifa hadi kwa upande wa klabu.
Tangu alipofunga bao kwenye mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Machi 23, 2022 hadi leo Samatta hajaifungia tena bao Taifa Stars katika mechi 14 alizoicheza.
Msimu huu amecheza mechi mbili tu za PAOK kwa dakika 40 na inaripotiwa kocha wa timu hiyo Răzvan Lucescu ameonyesha hana mipango naye kwa ajili ya msimu huu.
Katika msimu uliopita, Samatta alifunga mabao matatu katika mechi 44 za PAOK za mashindano tofauti.
Jana kocha Morocco alitangaza kikosi cha wachezaji 23 huku akitaja sababu tatu za uteuzi wa kikosi chake.
Alisema sababu hizo ni utimamu wa mwili kwa kila mchezaji, kiwango kwa sasa na vile wataendana na mipango yake kiufundi katika michezo hiyo ambayo ni dhidi ya Ethiopia na Guinea.
"Najua kuwa Watanzania wangependa kuona wachezaji wengi wa Kitanzania ambao wanacheza soka la kulipwa nje wakiitwa lakini lazima wajue kuwa sisi kama walimu kuna mambo ambayo huwa tunazingatia na wachezaji wapo wengi hivyo orodha ingekuwa ndefu,"
"Muda ni mchache sana kwa hiyo tumetazama wachezaji ambao wapo tayari moja kwa moja kuja kutumika, ni muhimu kuwa na wachezaji ambao wapo tayari sisi kama benchi la ufundi kazi yetu itakuwa kuingiza mbinu tu kwa ajili ya kutafuta matokeo katika michezo hiyo," amesema kocha huyo.
Wachezaji ambao wameitwa kwenye kikosi hicho makipa ni; Ally Salim (Simba), Aboutwalib Mshery (Yanga) na Yona Amos (Pamba).
Mabeki ni Nathaniel Chilambo, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo (Azam), Mohammed Hussein 'Tshabalala' (Simba), Dickson Job, Ibrahim Hamad 'Bacca', Bakari Mwamnyeto, Nickson Kibabage (Yanga), Abudlmalik Zakaria (Mashujaa).
Viungo ni Adolf Mtasingwa (Azam), Himid Mao (Talaal El Geish, Misri) Novatus Dismas (Goztepe, Uturuki), Mudathir Yahya (Yanga), Hussein Semfuko (Coastal Union), Edwin Balua (Simba) na Fiesal Salum (Azam)
Washambuliaji; Wazir Junior (Dodoma Jiji), Clement Mzize (Yanga), Cyprian Kachwele (Vancouver, Canada) na Abel Josiah (TDS TFF Academy.
Wachezaji hao wataingia kambini kuanzia Agosti 28 kwa ajili ya michezo hiyo.