Prime
MZEE WA FACT: Tungezitumia mechi hizi za FIFA kuwatafuta wachezaji wenye asili ya Tanzania
Kuelekea AFCON ya mwaka 2024 nchini Ivory Coast, kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Adel Amrouche, aliita kundi kubwa sana la wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaocheza sehemu mbalimbali duniani.
Wakaweka kambi Zanzibar na kuhitimisha kambi yao kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Zanzibar Heroes. Hapa ndipo tulipowaona akina Kwesi Kawawa , Tarryn Allarakhia na wengine.
Kwa Kawawa hatukufanikiwa lakini kwa Allarakhia tukapata mtu. Lakini baada ya pale, utamaduni huo ukaachwa moja kwa moja.
Jambo la busara lingekuwa kuendelea na utamaduni ule na kuokota mchezaji mmoja mmoja kila kinapokuja kipindi cha mapumziko ya FIFA.
Mwalimu wa timu ya taifa angepewa melekezo ya kuwaita wachezaji wanaocheza nje tu na ambao hawajawahi kucheza timu ya taifa, ili kutanua wigo wa kupata wachezaji...huku ligi inaendelea.
Jambo kama hili tukiwa tunalifanya mara kwa mara itatusaidia kuwapata wachezaji wengi wazuri. Hadi sasa tumepoteza wachezaji wengi ambao wangeweza kutusaidia kwenye timu ya taifa.
Ben Cabango:
Mzaliwa wa Wales kwa mama raia wa nchi hiyo na baba mtanzania. Anacheza nafasi ya beki wa kati akiitumikia klabu Championship ya Swansea City akiiwakilisha timu ya taifa ya Wales.
Anis Mehmeti:
Mzaliwa wa London Uingereza kutoka kwa mama mtanzania na baba raia wa Albania. Ni kiungo wa ushambuliaji akiichezea klabu ya Bristol City na kuiwakilisha timu ya taifa ya Albania.
Omar Richards:
Mzaliwa wa London kutoka kwa mzazi mmoja mtanzania na mmoja mjamaica.
Anacheza kama beki wa kushoto katika klabu ya Olympiacos ya Ugiriki na ameshachezea timu ya chini ya miaka 21 ya England. Bado hajachezea timu ya wakubwa. Tunaweza kumuwahi huyu.
Malik Tillman:
Mzaliwa wa Marekani kutoka kwa mama mtanzania na baba mmarekani. Ni kiungo wa ushambuliaji wa klabu ya PSV Eindhoven ya Uholanzi akiiwakilisha timu ya taifa ya Marekani.
Japhet Tanganga:
Mzaliwa wa London kutoka kwa wazazi wenye asili ya DR Congo lakini waliolowea kwanza Tanzania kabla ya kuzamia huko.
Ni mlinzi wa klabu ya Millwall akiiwakilisha England katika ngazi mbalimbali za vijana...hajacheza timu kubwa, tunaweza kumuwahi.
Hawa ni kwa uchache, kuna wachezaji wengi sana wenye asili ya Tanzania ambao tungeweza kuwawahi na kuwatumia kwenye timu ya taifa.
Hivi ndivyo Cape Verde wamefanya hadi wamefuzu Kombe la Dunia. Ndivyo Morocco wamefanya hadi kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia.
Lakini pia ndio msingi wa Senegal kufikia mafanikio yao ya sasa. Wakati wanajitafuta, walijenga timu yao kwa kuwategemea wachezaji wa aina hii.
Kile kikosi cha 2002 kilichocheza fainali ya AFCON na baadaye kufika robo fainali ya Kombe la Dunia, kilijengwa na akina Khalilou Fadiga, ambao ndio wachezaji wa aina hii.
Fadiga alienda kwenye Kombe la Dunia akiwa na uraia wa nchi tatu; Ubelgiji, Ufaransa na Senegal.
Kikosi cha Senegal liliitwa SeneF kwa sababu kilikuwa na wachezaji wenye asili ya Senegal ambao aidha walizaliwa Ufaransa au walikulia Ufaransa.
Mwaka huu Shirikisho la soka la kimataifa lilipanga kalenda yake ya matukio kwa mwaka ikiwa na vipindi vitano vya mapumziko ya mechi za kimataifa, vinne vya kawaida na kimoja cha Kombe la Dunia.
Machi 23 - 31 = Kawaida
Juni 1 - 9 = Kawaida
Juni 11 - Julai 19 = Kombe la Dunia
Septemba 21 - Oktoba 6 = Kawaida
Novemba 9-17 = Kawaida
Tanzania hatukufuzu kwa Kombe la Dunia, kwa hiyo hayo mapumziko hayatuhusu...tubaki na hayo mengine manne.
Tenga mapumziko mawili kwa ajili ya wachezaji wa aina hii ili kuwaona na kuwaingiza kidogo kidogo kwenye mfumo.
Tukifanya hivyo kwa miaka mitano tutabaini wachezaji wengi sana ambao watakuja kutusaidia sana huko mbeleni.
Lakini sisi Tanzania kwa kushindwa kwetu kufikiria vizuri, tukasimamisha ligi yetu ili tukitumie hiki kipindi cha Juni 1 -9.
Hili lilikuwa kosa kubwa sana. Ligi yetu imechelewa kumalizia kutokana na mambo mengi yaliyotokea kabla na wakati wa msimu, sasa badala ya kurekebisha kipindi hiki, tunazidi kuharibu.
Hakukuwa na ulazima wa sisi kucheza mechi hizi za sasa kwa sababu FIFA hailazimishi hilo.
FIFA wameacha wazo tarehe kwa anayetaka kutumia kutokana na uwezo na nafasi yake...sio lazima.
Kilicho lazima ni vilabu kuwaruhusu wachezaji wake kwenda timu ya taifa pindi wanapoitwa.
Kwa hiyo kwa kuwa wachezaji wengi hasa wa ligi kubwa kubwa duniani huitwa na nchi zao, ndio maana ligi hizo husimama.
Hii ni kwa sababu timu ikiwakosa wachezaji wake kuanzia watatu kwa kuitwa timu ya taifa, inaruhusiwa kutocheza mechi zake rasmi.