Nabi: Njooni mjifunze! amtaja Djuma, Lomalisa

KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi anacheeeeka.

Unajua kwanini? Beki wake wa kulia, Djuma Shaban amerejea mazoezi kutoka mapumzikoni, lakini kinachomfurahisha Nabi ni ufiti aliorudi nao staa huyo wa DR Congo. Achana na Djuma, Nabi anakoshwa pia na upande wa pili wa kushoto kwa beki, Joyce Lomalisa kuwa ni fundi kwelikweli akiwaambia wanaotaka kujifunza jinsi mabeki wa pembeni wanavyopaswa kucheza kisasa, basi waende wakajifunze kwa Mkongomani huyo aliyetua Yanga dirisha hili. Kuhusu Djuma unaambiwa, wakati akiwa mapumziko alikuwa anapiga tizi la kufa mtu, kitendo kilichomfurahisha Nabi kwani ni programu maalumu aliyopewa ili kumweka fiti zaidi.

Nabi alifunguka kazi aliyoifanya, Djuma msimu uliopita huenda ikaongezeka zaidi msimu ujao, huku pia beki wake mwingine akimfanya acheke tu.

Amefichua kuwa Djuma ndiye mchezaji mwenye nidhamu kubwa na kazi yake na baada ya kufanyiwa vipimo imegundulika alikuwa akifanya mazoezi makali kama alivyopewa programu maalumuakati timu hiyo ikifunga msimu.

Kutokana na programu hiyo, Nabi alisema Djuma amepunguza uzito wa mwili wake na kumfanya awe mwepesi zaidi na anaamini beki huyo atakuwa bora zaidi msimu na wapinzani wajipange.

“Watu wanaona kama alifanya kazi bora msimu uliopita, ni kweli lakini tunaomjua Djuma hakuwa katika ubora mkubwa ila msimu ujao atakuwa na moto mkubwa zaidi,” alisema Nabi na kuongeza.

“Tulimpa ratiba maalumu na masharti, anatakiwa kupunguza uzito, naweza kusema huyu ni mmoja ya watu bora wenye nidhamu ya kazi yao. amepungua na hata huku mazoezini ameanza kuwa Djuma ninayemjua.”

Mbali na Djuma, Nabi alifichua Lomalisa atawafundisha mabeki wengi jinsi ya kucheza kisasa.

Alisema amerudisha nguvu upande wa kushoto na msimu ujao nguvu yao ya kupandisha mashambulizi na kukaba itakuwa bora kupitia pembeni. “Kuna elimu ambayo mabeki wengine watajifunza jinsi ya beki wa kushoto anavyotakiwa kucheza, ashambulieje na akabe vipi, Lomalisa ni beki bora mtamwona na mtaelewa hakuja kujifunza.”