Namungo yaipa Simba mbinu kuiua de Agosto, rekodi yaibeba Yanga

Wednesday September 21 2022
namungo pic
By Ramadhan Elias
By Charity James

SIMBA, Yanga wamejipanga. Wametamka kwamba kuanzia raundi hii ijayo ya kwanza watafanya kazi kubwa zaidi ya ile iliyoonekana kwenye raundi ya awali ya mechi hizo za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba kupitia kwa kocha wao Juma Mgunda wamesisitiza kwamba timu yao imeanza kushika kasi na wanaamini kwamba ndani ya muda mfupi ujao iwe ndani au nje ya nchi mashabiki watafurahia zaidi.

Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu alisema kwamba wamejidhatiti na wataweka nguvu kubwa kwenye mechi ijayo dhidi ya Clube de Agosto ya Angola kuhakikisha watapata ushindi mnono na Mgunda bado ataendelea kuwa kocha mpaka itakapotangazwa vinginevyo.

Lakini Nabi Mohammed wa Yanga inayosubiri kuivaa Al Hilal ya Sudan, amesema wataingia kwenye mchezo huo kwa umakini mkubwa na wameanza kufanyia kazi mambo mbalimbali, huku akikiri kwamba juzi alikwenda Kwa Mkapa kuangalia mechi ya Simba kwavile anacheza nao Oktoba 23.


YANGA VS AL HILAL

Advertisement

Baada ya kuiondosha Zalan FC ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 9-0 katika mechi mbili nyumbani na ugeninini huku Fiston Mayele akitakata kwa kufunga hat-trick mara mbili, timu hiyo itakutana na kigogo kingine cha Sudan, Al Hilal yenye masikani yake katika mji wa Omdurman.

Hilal imefika hapo baada ya kuitoa Saint George ya Ethiopia kwa bao la ugenini baada ya kupoteza 2-1 ugenini na mechi ya pili kushinda 1-0 nyumbani.

Al Hilal inayonolewa na Kocha Florent Ibenge, haijawahi kabisa kukutana na Yanga kwenye michuano hiyo ya CAF, lakini zilishakutana mara tofauti katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), huku Yanga ikishinda mbili, ikipoteza mara moja na nyingine kuisha kwa sare.

Rekodi zinaonyesha timu hizo zilikutana mara ya kwanza mwaka 1988 katika mechi ya makundi ya michuano hiyo ya Kagame na Wasudan kushinda 2-0 kabla ya 1992 kukutana kwenye nusu fainali na Yanga kushinda kwa penalti 10-9 baada ya muda wa kawaida kumalizika kwa suluhu.

Miaka miwili baadaye timu hizo zilikutana tena katika mechi za makundi na kutoka sare ya 1-1 na mechi yao ya mwisho ilikuwa 1999 katika robo fainali na Yanga kushinda 2-1 na kutinga fainali kisha kwenda fainali kubeba ubingwa wa msimu huo kwa kuwafunga wenyeji SC Villa ya Uganda kwa penalti.

Kwa ukanda wa Cecafa, Hilal ndiyo timu yenye mafanikio makubwa katika historia ikiwa imefika fainali ya michuano ya CAF mara nyingi zaidi (5) ukilinganisha na klabu nyingine za ukanda huu.

Miaka michache iliyopita timu hiyo iliyumba kiuchumi lakini hivi karibuni imerejea kwenye uimara wake baada ya kupata mdhamini mpya aliyefanya kufuru kwenye usajili kwa kushusha mastaa kibao ikiwemo kocha Ibenge na lengo ikiwa ni kurudisha ubora wake.

Mechi ya kwanza itapigwa mwezi ujao kati ya Oktoba 7-9, 2022 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Yanga ikiwa nyumbani na mechi ya marudiano itachezwa Sudan kati ya Oktoba 14-17, 2022 na mshindi wa jumla atatinga makundi na atakayefungwa atadondokea Kombe la Shirikisho.


SIMBA VS PRIMEIRO DE AGOSTO

Simba iliyoiondosha Nyasa Big Bullets ya Malawi kwa jumla ya mabao 4-0, itakutana na Premiero De Agosto ya Angola iliyoiondosha Red Arrows ya Zambia kwa jumla ya mabao 2-1.

Agosto ina rekodi kubwa Afrika ikiwa imefika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2018 kabla ya kuyumba miaka mitatu iliyofuata kutokana na Janga la Corona sasa imeanza kujijenga taratibu na kurejea kwenye ubabe wake.

Agosto haijawahi kukutana na Simba hata mara moja iwe kwenye michuano ya CAF, wala kirafiki kitu kinachotoa picha timu hizo zikikutana pambano litakuwa gumu na lisilotabirika kirahisi.

Hata hivyo, bado Simba ina rekodi tamu dhidi ya timu zinazotoka Angola, kwani mwaka 1993 katika michuano ya Kombe la CAF iliitoa Atletico Sport Aviacao katika nusu fainali ya kutinga fainali na kucharazwa mabao 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast.

Hii Agosto ni ile iliyotolewa na Namungo kwenye Kombe la Shirikisho mwaka 2021 kwa jumla ya mabao 7-5 lakini imebadilika kila kitu kuanzia wachezaji, bajeti na ubora na sasa imeimarika zaidi.

Mechi ya kwanza Simba itakuwa ugenini kati ya Oktoba 7-9, 2022 nchini Angola na mechi ya marudiano itapigwa kwa Mkapa ambapo mshindi wa jumla atatinga makundi na atakayefungwa ataangukia Kombe la Shirikisho. Mangungu amesisitiza kwamba wameweka nguvu kubwa kwenye mashindano ya msimu huu na wana imani na Mgunda.


AZAM VS AL AKHDAR

Azam nayo ambayo haikucheza hatua ya mtoano ya awali kwenye Kombe la Shirikisho Afrika sasa itaanza katika hatua ya kwanza dhidi ya Al Akhdar SC kutoka Libya. Itacheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya TP Mazembe ugenini kujiweka sawa.

Akhdar imetinga hatua hiyo baada ya kuiondosha Al Ahli ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0 iliyoyapata kwenye mechi ya nyumbani baada ya kutoa suluhu ugenini.

Sio timu yenye jina kubwa katika michuano ya CAF lakini miaka ya hivi karibuni imekuwa na muendelezo mzuri hususani msimu huu na ni kati ya timu zinazotumia vyema uwanja wa nyumbani.

Azam na Akhdar hazijawahi kukutana na huenda ikawa mechi ngumu kwa pande zote mbili ambapo mchezo wa kwanza Azam itaanza ugenini kati ya Oktoba 7-9, mwaka huu na kurudiana Azam Complex Oktoba 14, 2022 na mshindi ataingia makundi.


KIPANGA vs CLUB AFRICAIN

Kipanga kutoka visiwani Zanzibar nayo imetinga hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho baada ya kuiondosha Al Hilal Wau ya Sudani Kusini kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2.

Huu unaweza kuwa mlima mrefu kwa Kipanga kutokana na rekodi na uzoefu mkubwa iliyonayo Club African kutoka Tunisia katika michuano yua CAF.

Watunisia hao ni mabingwa wa zamani wa Afrika wakitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa mwaka 1991 kwa kuifunga SC Villa ya Uganda mabao 7-3 katika fainali.

Hata hivyo, Kipanga licha ya kuzidiwa rekodi, ubora na vitu vingine vingi kwenye makaratasi na Africain, lakini mechi kati yao inatarajiwa kuwa ya aina yake kwani timu hizo mbili hazijawahi kukutana.

Mchezo wa kwanza Kipanga itakuwa nyumbani Oktoba kati ya Oktoba 7-9 na mechi ya marudiano itakuwa ugenini kati ya Oktoba 14-16.

Mchezaji wa zamani wa Mecco ya Mbeya, Abeid Kasabalala alisema; “Timu zote zimeanza vizuri zimeonyesha kuwa na kiu ya ushindi ari waliyomaliza nayo waendelee nayo ili waweze kutinga hatua inayofuata najua haitakuwa rahisi lakini wana kila nafasi ya kufanya vizuri ili waweze kufikia malengo.

“Mfano Yanga wameanza kwa ushindi mkubwa, timu imeonyesha uwezo japo wapinzani wao hawakuwa bora sana, lakini ndio mabingwa wa nchi waliyotoka. Kuelekea mechi inayofuata wanatakiwa kuongeza umakini hasa eneo la ushambuliaji ili kutumia kila nafasi watakayoipata ili kujitengenezea mazingira mazuri ugenini.

“Kwa upande wa Simba sina wasiwasi nao wao ni wazoefu wa mashindano na linapokuja suala la kuliwakilisha taifa wamekuwa wakionyesha ubora japo msimu huu wanatakiwa kuongeza nguvu zaidi ili kufanya vizuri, benchi la ufundi liongeze mbinu ili kufikia ubora wao wa misimu mitatu nyuma.”

Katibu Mkuu wa Namungo, Omary Kaaya ambaye aliiongoza timu ya Namungo msimu wa 2021 wakiiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikishio na kupata nafasi ya kucheza na De Agosto, alisema Simba ni wazoefu wa mashindano ya kimataifa wanafahamu fitna za mpira hivyo anaamini watakuwa wamejipanga.

“De Agosto ni watu wa fitna ni timu ya jeshi, Simba wanatakiwa kujipanga hasa kwenye suala la Covid watarajie kupimwa na jeshi la timu hiyo ambayo ndio inafanya mapokezi ya timu watakayokutana nayo. Kuhusiana na mechi ni timu nzuri wanatakiwa kujiandaa vizuri kwaajili ya ushindani,” alisema.

Advertisement