Ngoma kuikosa MO Bejaia

Donald Ngoma
Muktasari:
- Ngoma ataikosa mechi hiyo muhimu kwa Yanga kutokana na kuwa na kadi mbili za njano na kocha huyo Mholanzi amekiri kuwa ni pengo lakini hana wasiwasi kwani ana kikosi kipana na wapo watakaoziba nafasi yake.
Dar es Salaam. Pamoja na kumkosa mshambuliaji wake tegemeo Donald Ngoma katika mchezo ujao dhidi ya MO Bejaia, kocha wa Yanga, Han Pluijm anaamini bado anayo nafasi ya kucheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ngoma ataikosa mechi hiyo muhimu kwa Yanga kutokana na kuwa na kadi mbili za njano na kocha huyo Mholanzi amekiri kuwa ni pengo lakini hana wasiwasi kwani ana kikosi kipana na wapo watakaoziba nafasi yake.
Akizungumza na gazeti hili, Pluijm alisema hakati tamaa mpaka mechi ya mwisho kwani bado anamini lolote linaweza kutokea huko mbele na bado wanaweza wakashangaza ulimwengu kwa kutinga nusus fainali.
Yanga haipewi nafasi ya kufuzu kwa nusu fainali baada ya kupoteza michezo mitatu na kutoa sare mmoja hivyo kushika mkia kwenye Kundi A ikiwa na pointi moja, huku TP Mazembe ya DR Congo ikiongoza na pointi 10, ikifuatiwa na MO Bejaia ya Algeria yenye pointi tano sawa na Medeama ya Ghana.
Kama Yanga inataka kutinga nusu fainali inatakiwa iifunge MO Bejaia katika mchezo ujao utakaofanyika Agosti 13 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuomba TP Mazembe iichape Medeama.
Iwapo Yanga itaifunga MO Bejaia itafikisha pointi nne na ikiwa Mazembe itaifunga Medeama itafikisha pointi 13 na itakuwa imeshakata tiketi ya kutinga nusu fainali huku Medeama na MO Bejaia zikibakiwa na pointi tano.
Hivyo, Yanga itakuwa na kazi moja tu ya kuhakikisha inashinda mechi ya mwisho dhidi ya TP Mazembe ili ifikishe pointi saba wakati ikiomba MO Bejaia na Medeama zitoke sare tu ili zifikishe pointi sita.
Kama Yanga itapoteza mchezo ujao dhidi ya MO Bejaia itakuwa imepoteza matumaini ya kutinga nusu fainali kwani Bejaia itafikisha pointi nane ambazo haziwezi kufikiwa na mabingwa hao wa Tanzania.
Pia, hata kama Yanga itaifunga MO Bejaia na Medeama ikaifunga TP Mazembe basi Yanga itakuwa tayari haina nafasi ya kuingia nusu fainali kwani Medeama itafikisha pointi nane ambazo Yanga haiwezi kuzifikia hata kama itashinda mchezo wake wa mwisho.
Pluijm alisema hivi sasa wanafanya mazoezi, huku wakirekebisha makosambalimbali yaliyojitokeza katika mchezo uliopita dhidi ya Medeama.
“Tunaendelea na mazoezi na kuangalia wapi tulikosea na kurekebisha kabla ya mchezo ujao, bado tuna matumaini, hakuna kukata tamaa mpaka mechi ya mwisho.”
Wakati huohuo; MO Bejaia imepata pigo kwa kuwakosa wachezaji wake wawili beki Adel Lakhdari na kiungo Ferhat Malek kwenye watakaoukosa mechi dhidi ya Yanga kutokana na kupata kadi mbili za njano