Ni siku ya hukumu Ligi Kuu Bara

Mchezaji nyota wa Azam, Feisal Salum na mchezaji nyota wa Yanga, Aziz KI

Dar es Salaam. Ni siku ya hukumu! ndivyo unavyoweza kuizungumzia Jumanne ya leo wakati pazia la Ligi Kuu ya NBC 2023/2024 litakapofungwa rasmi kwa mechi nane zitakazochezwa kwenye viwanja na miji tofauti nchini kuanzia saa 10:00 jioni.

Maswali na matarajio tofauti ambayo wadau na mashabiki wa soka wamekuwa nayo kwa muda mrefu yote yatapata majibu yake baada ya kukamilika kwa dakika 90 kwenye mechi hizo ambazo zote zitachezwa kwa muda mmoja ili kuepuka upangaji wa matokeo, huku mambo manne yakiwavuta zaidi mashabiki.

Mechi hizo nane zinazochezwa leo na viwanja vyake kwenye mabano ni Yanga dhidi ya Tanzania Prisons (Azam Complex), Simba na JKT Tanzania (Benjamin Mkapa), Mashujaa na Dodoma Jiji (Lake Tanganyika), Ihefu na Mtibwa Sugar (Liti), Coastal Union na KMC (Mkwakwani), Namungo na Tabora United (Majaliwa), Geita Gold na Azam (Nyankumbu) na Singida Fountain Gate dhidi ya Kagera Sugar (CCM Kirumba).

Tayari Yanga imeshakabidhiwa taji la ligi hiyo ikiwa na pointi 77 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote kwenye ligi hiyo msimu huu wakati Mtibwa Sugar imeshuka daraja kwa kuwa na pointi ambazo hazitoshi kuifanya imalize juu ya nafasi mbili za mwisho kama inavyofafanua kanuni ya sita, ibara ya pili ya Ligi Kuu msimu huu.

"Timu mbili (2) za mwisho, zilizoshika nafasi ya 15 na 16 kwenye Ligi Kuu

zitashuka moja kwa moja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (Championship)

msimu unaofuata," inafafanua ibara hiyo.

Azam, Simba kumaliza ubishi

Timu moja itakayoungana na Yanga kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kwa kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kati ya Azam na Simba itajulikana leo pamoja na ile itakayoungana na Coastal Union kucheza Kombe la Shirikisho Afrika kwa kumaliza ikiwa katika nafasi ya tatu.

Timu hizo mbili kila moja imekusanya pointi 66 lakini Azam FC iko nafasi ya pili kutokana na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa ilionao kulinganisha na Simba kigezo ambacho ni cha kwanza kutumika kuamua timu mshindi katika nafasi tofauti ikiwa timu mbili zimelingana pointi.

"Endapo timu zitalingana pointi mshindi itakuwa timu iliyo na tofauti bora

ya magoli ya kufunga na kufungwa (goals difference)," inafafanua ibara ya nne ya kanuni ya nane ya ligi kuu msimu huu.

Hadi sasa, utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa wa Azam ni mabao 40, ikiwa imefunga 61 na kufungwa 21 wakati Simba ikiwa nayo 32 ambapo imeweka kimiani mabao 57 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 25.

Ili Simba imalize katika nafasi ya pili, inapaswa kushinda mechi yake dhidi ya JKT Tanzania na kisha kuombea Azam FC ipoteze au kutoka sare dhidi ya Geita Gold, au ipate ushindi wa idadi kubwa ya mabao ambayo yatafanya ivuke tofauti ya mabao nane ya kufunga na kufungwa ambayo imezidiwa na Azam.

Kocha wa Simba, Juma Mgunda alisema kuwa bado wana matumaini ya kumaliza katika nafasi ya pili ambayo ili yawe hai, ni lazima wapate ushindi dhidi ya JKT Tanzania.

"Tunahitaji ushindi kwenye mchezo wa kesho (leo) kwani ni mechi yenye maamuzi ili kuona msimu huu tutamaliza vipi. Wachezaji wote wanafahamu hilo na wapo tayari kutimiza malengo yetu," alisema Mgunda.

Bruno Ferry wa Azam FC alisema kuwa wanahitaji kumaliza katika nafasi nzuri na hawataidharau Geita Gold.

"Geita hawapo katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi lakini hilo haliwezi kutufanya tubweteke na kuona mechi itakuwa rahisi kwa upande wetu. Tunapaswa kucheza vyema ili tupate ushindi na kumaliza vyema ligi," alisema Ferry.


Geita Gold, Tabora presha tupu

Kama kuna timu zipo kwenye presha kubwa leo ni Geita Gold ambayo itakuwa nyumbani kucheza na Azam FC na Tabora United ambayo itakuwa ugenini kukabiliana na Namungo FC.

Kupoteza au sare dhidi ya Azam FC kutafanya Geita Gold kushuka rasmi daraja lakini inaweza pia kushuka hata ikipata ushindi, iwapo Tabora itaibuka na ushindi mbele ya Namungo huko Ruangwa, Lindi.

Tabora United inaweza kushuka daraja ikiwa itapoteza au kutoka sare dhidi ya Namungo na Geita kushinda dhidi ya Azam.


Vita ya timu saba

Timu saba zimekwepa kushuka daraja moja kwa moja lakini leo hapana shaka kila moja itakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha haimalizi ama katika nafasi ya 13 au ya 14 itakayofanya icheze mechi za mchujo (play off) za kuwania kubaki Ligi Kuu.

Orodha hiyo ya timu sana inazijumuisha, Namungo, Ihefu Singida Fountain Gate na Dodoma Jiji zenye pointi 33 kila moja, Mashujaa na JKT Tanzania ambazo kila moja ina pointi 32 na Kagera Sugar iliyo na pointi 31.

Matokeo ya sare tu, yanatosha kuzibakisha ligi kuu, Namungo, Ihefu, Singida Fountain Gate na Dodoma Jiji, Mashujaa na JKT Tanzania kwani Kagera Sugar na Tabora United zilizo katika nafasi ya kucheza mchujo wa kuwania kubaki Ligi Kuu, hazitoweza kufikia pointi zao.

Kagera Sugar yenyewe inalazimika kuibuka na ushindi dhidi ya Singida Fountain Gate leo ili ifikishe pointi 34 zitakazotosha kuifanya ibaki ligi.


Ufungaji bora ni Fei Toto ama Aziz Ki

Ushindani wa kupata mfungaji bora wa Ligi Kuu leo pia utafikia tamati ambapo mmoja kati ya Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam FC na Stephane Aziz Ki ni lazima aibuke mshindi.

Wawili hao wamefunga idadi sawa ya mabao ambapo kila mmoja amefumania nyavu mara 18 na kwa mujibu wa kanuni, iwapo watalingana hadi mwisho, vigezo vinne vitatazamwa kwa kuanzia na utofauti wa alama zitakazopatikana kwa mabao yaliyofungwa kwa njia ya penalti na yale ya kawaida.

"Mshindi wa tuzo ya Mfungaji Bora ni mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kuliko wengine katika shindano husika. Ikitokea wachezaji zaidi ya mmoja wamefungana idadi ya mabao, vigezo vifuatavyo vitatumika kwa kufuata mpangilio ili kumpata mshindi.

"13.1 Magoli yaliyofungwa kwa njia ya kawaida yatakuwa na alama mbili (2) na magoli yaliyofungwa kwa njia ya penati yatakuwa na alama moja (1). Mchezaji mwenye alama nyingi atakuwa mshindi. 13.2 Endapo watalingana alama, mchezaji aliyecheza muda mchache zaidi atakuwa mshindi.

Kwa kigezo cha mabao ya penalti ambacho kinaanza, Fei amefunga moja huku Aziz Ki akifunga matatu, hivyo kama mambo yakibaki hivi nafasi kubwa itakuwa kwa kiungo huyo wa Azam.

"13.3 Endapo watafanana katika vigezo vyote viwili hapo juu, mchezaji aliyefunga mabao mengi ugenini atakuwa mshindi. 13.4 Katika mashindano ya mtoano, Mshindi atakuwa mchezaji ambaye timu yake imefika hatua ya juu zaidi kuliko mwingine na endapo hatua hii haitatoa mshindi kipengele cha i-iii vitatumika kwa mpangilio wake," inafafanua kanuni ya kumi na moja ibara ya 13.


Diarra, Matampi wana jambo lao

Ni mechi ambazo pia zinaweza kutoa uamuzi wa kipa ambaye amecheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao kati ya Djigui Diarra wa Yanga na Ley Matampi wa Coastal Union.

Wawili hao kila mmoja amecheza mechi 13 msimu huu bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.