Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nyosso akaliwa kooni

Juma Nyosso

Muktasari:

Nyosso msimu uliopita alifungiwa mechi nane kutokana na kumdhalilisha Maguli.

Dar es Salaam. Wadau mbalimbali wa soka nchini wameonyesha kuchukizwa na kitendo cha beki, Juma Nyosso kumdhalilisha mshambuliaji, John Bocco katika pambano kati ya Azam na Mbeya City lililofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini juzi.

Katika pambano hilo, Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 yaliyofungwa na Kipre Tchetche na Mudathir Yahaya wakati bao la Mbeya City lilifungwa na Rafael Alpha.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia kwa rais wake, Jamal Malinzi limeelezea kusikitishwa kwake na kitendo kilichofanywa na Nyosso huku likisema kuwa linajiandaa kumchukulia hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine wenye tabia kama yake.

“TFF kwanza inasikitishwa na udhalilishaji uliofanywa na yule mchezaji kwa mwenzake, lakini pili tuwahakikishie wapenzi wa soka na Watanzania kwa ujumla kuwa shirikisho litamchukulia hatua kali za kisheria ndani ya muda mfupi ili kukomesha vitendo vya namna ile,” alisema Malinzi.

Kwa mujibu wa kanuni za TFF,  kosa la Nyosso ni kinyume na kanuni namba 37(24) ya Ligi Kuu inayohusu udhibiti wa wachezaji inayosema, “Mchezaji yeyote atakayepatikana na hatia ya kufanya makosa makubwa ya kimaadili au kinidhamu, au ya kibaguzi au ya kidhalilishaji au yatakayotafsiriwa kuwa ni ukiukaji mkubwa wa taratibu za mchezo na ubinadamu atatozwa faini kati ya Sh 1 milioni mpaka Sh 3 milioni au kusimamishwa kushiriki michezo mitatu mpaka kumi ya klabu yake yoyote atakayoitumikia katika Ligi Kuu  na mashindano mengine rasmi ya TFF au kufungiwa kipindi cha kati ya mwaka mmoja na miwili.”

Hii si mara ya kwanza kwa Nyosso kujihusisha na matukio yanayoashiria utovu wa nidhamu uliopitiliza pindi anapokuwa uwanjani. Januari 28, mwaka huu Nyosso alifanya kitendo kama hicho kwa mshambuliaji Elias Maguli wakati Mbeya City ilipocheza dhidi ya Simba ambapo beki huyo alijikuta akifungiwa kucheza jumla ya mechi nane za Ligi Kuu. Mwenyekiti wa Chama  cha Wachezaji wa Soka Tanzania (Sputanza), Musa Kissoky amelaani kitendo cha Nyosso huku akiiomba TFF impe adhabu kali itakayoendana na ushauri nasaha kwa mchezaji huyo ambaye hii si mara ya kwanza kufanya kitendo kama hicho.

“Huyu kijana amefanya kitendo cha aibu ambacho si mara ya kwanza kwake kukifanya. Sisi kama Sputanza tunaiomba TFF itoe adhabu kali kwake ili iwe fundisho kwa wengine.”

“Pia anatakiwa apelekwe kwa wanasaikolojia ili waweze kufahamu ana tatizo gani hasa kwa sababu inaweza kuwa ana matatizo.  Kwa sababu tabia ya mtu inaendana na aina ya malezi aliyokulia,” alisema Kissoky.

Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi alisema amelisikia suala hilo, lakini anahitaji muda wa kulifuatilia kwa undani kabla ya kulitolea uamuzi.

“Tupo njia tunaenda Mwanza, nimesikia suala la Nyosso, lakini kwa sasa siwezi kuliongelea hadi nitakapofanya uchunguzi na kupata ushaidi mzuri wa kulisemea suala hili,” alisema Mwambusi.

Msemaji wa Azam FC, Jaffar Idd alisema klabu yake imesikitishwa na kitendo hicho, lakini haiwezi kufanya chochote juu ya suala hilo kwa vile limeshafika mikononi mwa vyombo husika.

“Jambo hili tayari lipo kwenye mikono ya shirikisho ambalo lina taratibu zake za kutoa uamuzi wa masuala ya kisoka. Kama Azam FC hatuwezi  kuingilia majukumu ya TFF ambayo tayari inalishughulikia suala hili,” alisema Idd.