Rais Mwinyi aipa zawadi Zanzibar Heroes Sh50 milioni

Muktasari:
- Ni mwaka wa tatu mfululizo kombe la Mapinduzi linabaki kisiwani humo baada ya Januari 13, 2025 Zanzibar Heroes kuifunga Burkina Faso 2-1 katika uwaja wa Gombani Pemba na kujinyakulia kitita cha Sh100 milioni.
Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi ameizawadia timu ya Taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' Sh50 milioni baada ya kutwaa kombe la Mapinduzi 2025.
Akizungumza katika hafla maalumu ya chakula cha mchana alichoandaa kwa ajili ya wachezaji wa timu hiyo katika viwanja vya Ikulu leo Januari 15, 2025, Rais Dk Mwinyi amesema timu hiyo imeiletea heshima kubwa Zanzibar na kudhihirisha uwapo wa vipaji vingi vya soka vinavopaswa kuendelezwa.
"Kwa mafanikio ya Zanzibar Heroes kuna kila sababu kwa Serikali kuendelea na ujenzi wa Academy za soka kila Mkoa kwa lengo la kuviibua vipaji vya vijana," amesema
Amesema tayari wagunduzi wa vipaji vya soka (SCOUT) wa nchini Uturuki wameonesha nia ya kuja Zanzibar baada ya kuushuhudia mchezo wa fainali baina ya Zanzibar na Burkinafaso na kukiri kuwepo vipaji vingi.
Kutokana na hali hiyo, Dk Mwinyi ametangaza dhamira ya kuunda kamati maalumu ya kitaifa hivi karibuni itakayokuwa na jukumu la kumshauri namna bora ya kuuendeleza mpira wa miguu hapa nchini.
Alisema kamati hiyo itaweza kupendekeza kwake jinsi gani ya kulifanya soka la Zanzibar kuwa bora zaidi.
Amesem kamati hiyo itakuwa na wabobezi katika masuala ya michezo ili waweze kumpa ushauri mzuri lakini pia na madhumuni ya kuwa na timu imara zaidi kutoka chini hadi taifa.
“Kamati hii nitaitangaza hivi karibuni ili ianze kazi mara moja ya kushauri,” alisema.
Dk Mwinyi akizungumzia ushindi uliopatikana katika fainali ya mashindano ya Mapinduzi Cup kwa timu ya Zanzibar Heroes kupata ushindi wa bao 2-1 dhidi ya timu Burkina Faso amesema inaonekana Zanzibar ina kiwango kikubwa cha mpira wa miguu kutokana na ushindi unaopatikana.
“Kwanini nasema hivyo, kwasababu under 15 walishinda na walichukua Kombe wakalileta hapa Zanzibar, Mlandege mara mbili mfululizo katika mashindano ya Mapinduzi wamelibakisha Kombe la hapa na mara hii Zanzibar Heroes katika timu za taifa wamelibakisha Kombe Zanzibar,” alisema.
Amesema "wengi wetu tuliposikia kwamba zinakuja timu kutoka East Afrika tukasema wao ndio watapata ushindi lakini huku tukijua kwamba uzalendo wetu na jinsi tunavyopigana kwenye jambo la kitaifa tunaweza kufanya vizuri na kweli hilo wamelidhihirisha na sote tulifurahi,."
Naye Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, amesema mwaka huu walipata changamoto kubwa, wadhamini wengi walikuwa wanabana kutokana na Imani kuwa wakiwekeza fedha zao Pemba hawatapata faida.
“Tulikuwa tuna kazi kubwa ya kuelimisha lakini mpaka dakika za mwisho wadhamini hawakutoa na walituahidi ili jambo kwa kweli limedhorotesha baadhi ya mambo katika Kombe la Mapinduzi,” alisema.
Naye Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Suleiman Mahmoud Jabir alimpongeza Rais Mwinyi kwa kuwathamini na kusherehekea ushindi kwa timu yao wakiwa mabingwa kwa mwaka 2025 kwa kombe la Mapinduzi.
"Tumeionesha dunia kama Zanzibar tuna vipaji na kama tutapata fursa na kupata nafasi katika mashindano ya kimataifa naamini kabisa tunaweza kufanya makubwa na mazito zaidi," alisema.
Hemed Suleiman Moroko ni Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Zanzibar Heroes, alisema Zanzibar ina vipaji vikubwa na anaamini itafika mbali katika sekta ya michezo.
Alimkabidhi Rais Mwinyi timu hiyo na kumuomba kuwanunulia vifaa vya kisasa ikiwemo kifaa cha kipima masafa GPS.
Pamoja na kukabidhiwa kiasi hicho Cha fedha wengine waliowapa zawadi na fedha zao kwenye mabano ni Baraza la Wawakilishi (Sh10 milioni), PBZ (Sh10 milioni), CRDB (Sh15 milioni na Rahisi Solution (Sh10 milioni).