Shilton arudishwa Simba

KOCHA wa zamani wa makipa wa Simba, Mohammed Mharami ‘Shilton’ amerudishwa Msimbazi kwa sasa akiunda benchi la ufundi la timu hiyo ambayo jana jioni ilikuwa uwanjani kumalizana na Nyasa Big Bullets ya Malawi katika mechi ya marudiano ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Licha ya mabosi wa Simba kufanya siri, lakini Mwanaspoti linafahamu, Shilton tayari ameanza kazi Msimbazi akiwanoa makipa wa timu hiyo wakati ikijiandaa na mechi ya jana iliyopigwa Kwa Mkapa.

Shilton aliondolewa Simba mwishoni mwa mwaka juzi na nafsi yake kuchukuliwa na Milton Nienov aliyepo Yanga kwa sasa. Shilton anaungana na kocha wa mpito, Juma Mgunda na wasaidizi wake, Seleman Matola na Sebastian Nkoma aliyetua wiki iliyopita, Simba ilipojiandaa kucheza ugenini na Big Bullets.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema, Shilton amechukuliwa ili kuliongezea nguvu benchi baada ya kuondoka kwa Zoran Maki na wasaidizi wake akiwamo kocha wa makipa, Mohammed Rachid na yule wa viungo, Sbai Karim walioenda kuinoa Al Ittihad ya Misri.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally alipoulizwa jana kwa njia ya simu alijibu kwa kifupi: “ Sina la kusema kwani akili yetu kwa sasa ipo kwenye mechi dhidi ya Big Bullets.”