Silva atupa taulo kufuatia kipigo cha Madrid
Muktasari:
- Silva amesema hali ya timu yake kwa sasa ni ngumu kutokana na kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao.
Madrid, Hispania. Nahodha wa Manchester City, Bernardo Silva, amesema matumaini ya timu yake kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya yako katika hali ngumu baada ya kupokea kichapo kizito cha mabao 3-0 dhidi ya Real Madrid.
Katika mchezo wa hatua ya 16 bora uliopigwa katika dimba la Santiago Bernabéu, Madrid, Hispania wenyeji waliibuka na ushindi huo uliotokana na mabao matatu ya kiungo wao Federico Valverde.
Matokeo hayo yanaiacha Man City na kazi kubwa katika mchezo wa marudiano utakaochezwa wiki ijayo kwenye uwanja wa Etihad.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Silva amesema hali ya timu yake kwa sasa ni ngumu.
Nahodha wa Manchester City, Bernardo Silva, akionekana kuelekeza jambo katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid. Picha na Mtandao
“Ukiwa nyuma kwa mabao 3-0 inakuwa vigumu zaidi. Kwa sasa tunajisikia vibaya sana, ni kama giza. Lakini kesho ni siku nyingine, na wiki ijayo tutaingia uwanjani tukiamini bado tuna nafasi,” amesema Silva.
Silva ameongeza kuwa timu yao ilianza mchezo vizuri lakini walipoteza mwelekeo baada ya kufungwa bao la kwanza.
“Tulianza vizuri na tulikuwa tunapata nafasi sahihi. Lakini baada ya kufungwa bao la kwanza tulipoteza udhibiti wa mchezo. Tulishindwa kudhibiti mashambulizi ya kushtukiza. Ukicheza dhidi ya Real Madrid lazima ulipe gharama kwa makosa hayo,” ameeleza.
Katika mchezo huo, kipa wa Man City, Gianluigi Donnarumma aliokoa penalti ya mshambuliaji Vinícius Júnior kipindi cha pili, jambo lililozuia Madrid kuongeza mabao zaidi.
Kwa upande wake, kocha wa Man City, Pep Guardiola amekiri kuwa matokeo hayo ni mabaya lakini akaahidi timu yake itapambana katika mchezo wa marudiano.
Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, akionekana kukazia jambo kuelekea kwa wachezaji wake katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid. Picha na Mtandao
“Matokeo ya 3-0 si mazuri, hatuwezi kuyaficha. Tulishindwa kudhibiti mashambulizi. Hata hivyo tutajaribu kupambana wiki ijayo mbele ya mashabiki wetu,” amesema Guardiola.
Guardiola pia amekanusha madai kuwa alifanya majaribio mengi ya kimfumo kwa kuanza na wachezaji wa pembeni Jérémy Doku, Savinho na Antoine Semenyo.
Katika upande wa Madrid, beki wa kulia Trent Alexander-Arnold amempongeza Valverde kwa kiwango chake bora akisema ni miongoni mwa wachezaji wanaopuuzwa licha ya mchango wake mkubwa.
Nahodha wa Real Madrid, Federico Valverde (kulia), akishangilia moja ya bao alilofunga kati ya matatu yaliyoipa Madrid ushindi dhidi ya Manchester City, mwingine kushoto ni nyota wa timu hiyo Vinicius Jr. Picha na Mtandao
“Valverde ni mchezaji wa ajabu. Anakimbia kila sehemu ya uwanja na anatoa kila kitu kwa ajili ya timu. Ni mmoja wa wachezaji wanaopuuzwa zaidi duniani,” amesema Alexander-Arnold.
Ushindi huo umeiweka Madrid katika nafasi nzuri ya kutinga robo fainali, huku City wakihitaji ushindi mkubwa katika mchezo wa marudiano ili kubadili matokeo.
Katika michezo mingine ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa jana, ilishuhudiwa PSG ikiichapa Chelsea mabao 5-2, Arsenal ikiwa ugenini iliambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Bayer Leverkusen wakati Bodo/Glimt ikiendelea kuonyesha ubora kwa kuifunga mabao 3-0 Sporting CP ya Ureno.