Simba imeanza kuiva- Robertinho

Dar es Salaam. Licha ya kupoteza kwa mabao 3-1 katika mechi ya mwisho ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca usiku wa kuamkia jana, kocha wa Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ ametamba siku za neema Msimbazi zinakaribia kutokana na kuongezeka na kuimarika kwa ubora timu hiyo siku hadi siku tangu alipojiunga nayo.

Kichapo hicho hakikubadilisha chochote katika msimamo wa kundi C kwani Raja Casablanca ilimaliza ikiwa kinara na Simba ikibaki nafasi ya pili, lakini Robertinho anaamini kikosi chake kilivyocheza kimeonyesha kinampa matumaini kuwa ndoto za kukifikisha nchi ya ahadi ambayo ni hatua za juu za mashindano ya klabu Afrika na ikiwezekana kutwaa mataji zinakaribia.

“Nina miezi minne hapa lakini hii timu itakuwa imara zaidi siku chache zijazo. Timu inacheza vizuri ikiwa na mpira na hata isipokuwa nao.

“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kucheza vizuri ingawa tumepoteza kwa mabao matatu, ilikuwa mechi nzuri Raja ni timu bora,” alisema Robertinho.

Kocha huyo alisema kwa sasa akili zao wanazielekeza katika mechi ya robo fainali ambayo ametamba wako tayari kukabiliana na timu yoyote ambayo watapangwa kucheza nayo.

“Hatua ya makundi imeisha na sasa kilichopo mbele yetu ni robo fainali ambayo hapana shaka itakuwa ngumu zaidi, lakini hilo halitupi wasiwasi na tutakuwa tayari kucheza na yeyote tutakayekutanishwa naye. Hii ni hatua ambayo haina timu rahisi. Zote ni ngumu na zenye ubora hivyo tunapaswa kujiandaa vilivyo,” alisema.

“Kila hatua unayofika ndio ugumu unaongezeka na ili ufanye vizuri ni lazima ukutane na wapinzani walio bora na uonyeshe ubora wako.”

Simba inasaka tiketi ya kutinga nusu fainali ya mashindano ya klabu Afrika kwa mara ya kwanza tangu muundo wa mashindano hayo ubadilike 2017 baada ya kuishia robo fainali mara tatu tofauti katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Katika mara hizo tatu ambazo Simba ilifika robo fainali na kukomea hapo, mara moja ilitinga ikiwa kinara wa kundi na mara nyingine mbili ilikuwa baada ya kumaliza ikiwa nafasi ya pili kwenye kundi lake.

Droo ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu imepangwa kuchezeshwa Aprili 5 jijini Cairo ambapo Simba inategemewa kukutanishwa na timu mojawapo kati ya tatu ambazo zitakuwa vinara kwenye kundi A, B na D la mashindano hayo.