Simba kuvunja rekodi

Thursday September 23 2021
simbapic
By Imani Makongoro

Watani wa jadi, Simba na Yanga Jumamosi watacheza mechi yao ya 24 katika kipindi cha miaka 10, wakiwania ngao ya hisani kwenye uwanja wa Mkapa Dar es Salaam, mechi ambayo Simba itakuwa na kibarua cha kupambana kuivunja rekodi ya Yanga ya miaka 10 kinyume na hapo Yanga itaendelea kuwa kinara kwa kipindi hicho.

Mechi hiyo ya watani itakuwa ni ya tatu kuchezwa mwaka huu, baada ya ile ya Ligi ya mzunguko wa pili msimu uliopita ya Julai 3 na ile ya fainali ya FA ya Julai 25 ambazo timu hizo ziligawana ushindi wa bao 1-0 katika kila mechi.

Jumamosi ijayo, timu hizo zitakutana kwa mara ya 24 katika kipindi cha miaka 10 kwenye mechi za Ligi, FA na Cecafa tangu ile ya, Machi 5, 2011 ambayo ilimalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1 kwenye Ligi msimu wa 2010/11.

Katika mechi 23 walizocheza, Yanga imefunga mabao 23 na Simba mabao 22 huku Yanga ikiwa na rekodi ya kuifunga Simba mara nyingi zaidi kwenye mechi hizo, ikiwamo mbili za Septemba 30, 2018 na Septemba 26, 2015 ambapo Yanga ilishinda bao 2-0 na moja zilisuluhu.

Mechi hiyo ambayo uwagawa mashabiki wa soka, haijawacha salama nyota wa zamani wa timu hizo ambao kila mmoja anaamini yake itachomoza na ushindi, huku baadhi ya wadau wakibaiisha itaamuliwa na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja kwani haitabiriki na iko nusu kwa nusu kwa pande zote.

Simba na Yanga ambazo hivi karibuni zimetoka kufungwa, Yanga ikichapwa bao 1-0 na Rivers nchini Nigeria na kuondoshwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba kuambulia kipigo kama hicho kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya TP Mazembe zimeingia kambini jana kujiandaa na mechi hiyo ambayo ndiyo habari ya mjini kwa sasa.

Advertisement

“Naipa asilimia 70 za ushindi Simba kutokana na maandalizi waliyoyafanya kwenye pre season na aina ya wachezaji ilionao,” alisema kipa wa zamani wa timu hiyo Moses Mkandawire.

wakati Makumbi Juma ‘Homa ya jiji’ nyota wa zamani wa Yanga akiipa ushindi timu yake hiyo ya zamani Jumamosi.

“Simba na Yanga uwa ni mechi ya kufa na kupona kwa Yanga, hata saikolojia za wachezaji zinabadilika, ninachokitarajia ni ushindi tu kwa timu yangu, Simba haitusumbui,” alijinasibu Makumbi.

Kipa mwingine wa Yanga na Stars, Juma Pondamali alisema mechi hiyo itaamuliwa na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na mbinu za makocha.

“Pamoja na changamoto ambazo Yanga inapitia kipindi hiki, lakini inapofikia mechi ya watani, hata maandalizi yanakuwa ni tofauti, ni mechi ambayo kwa asilimia 99 haitabiriki,” alisema.

Katika mchezo huo, Simba itakuwa na kibarua cha kusawazisha ili kuwa sawa na Yanga ambayo kwa miaka 10 iliyopita inaongoza kwa ushindi dhidi ya Simba.

Katika mechi hizo, Yanga imeshinda mechi saba kwa ushindi bao 1-0 mara nne na mabao 2-0 mara tatu.

Simba yenyewe imeshinda mara sita, huku ikiwa na historia ya ushindi mnono wa mabao 5-0 katika kipindi hicho na kipigo cha bao 1-0 katika mechi nne ikiwamo ya karibuni ya FA, ushindi wa bao 2-1.

Timu hizo zimetoka sare katika mechi 10, ambazo ni za mabao 1-1 mara sita, suluhu mara mbili na sare ya mabao 2-2 a ile ya mabao 3-3.

Mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema mechi hiyo iko nusu kwa nusu kwa timu zote.

“Hata wachezaji uwa wanazichukulia kwa upekee na kujiandaa kwa upekee nje ya mazoezi yao ya kawaida, ni mechi ambayo binafsi naiona itaamuliwa na uwezo wa mchezaji binafsi,” alisema.

Kocha msaidizi wa Simba Queens, Maty Mseti alisema katika mchezo huo, Yanga wanaweza uingia na hamasa kubwa hasa baada ya kupoteza mechi zao mbili za kimataifa hivi karibuni na Simba kwa kujiamini kwao wakafungwa.

“Niliiangalia Simba kwenye mechi na Mazembe midifidi yake ilikatika, na alikosekana mtu wa kuamua matokeo kama alivyokuwa Chama ‘Clatous’, ikitokea hivyo Jumamosi na ukizingatia Yanga ina mtu wa kuposesi mpira kama Fei toto ‘Feisal Salum’ lolote linaweza kutokea,” alisema.

Advertisement