Simba yadondosha pointi mbili Mbeya

Mbeya. Dakika 90 za mechi ya Mbeya City imemalizika kwa timu hizo kutoa sare ya bao 1-1 huku mabao ya Mzamiru Yassin (Simba) na Tariq Seif yakitosha kumaliza mtanange huo.


Hizi ni dondoo za mechi hiyo;

Bao la Mzamiru Yassin alilofunga linakuwa la pili kwake msimu huu na kufikisha mabao 30 kwa Simba kuihenyesha Mbeya City waliofikisha mabao saba .

Katika dakika 90 za mchezo huo Simba ilipata kona saba kwa mbili huku mchezaji wa Mbeya City, Hassan Mohamoud akioneshwa kadi ya njano dakika ya 38 baada ya kumchezea rafu Moses Phiri.

Simba inashindwa kulipa kisasi kwani msimu uliopita ikicheza uwanjani hapo Sokoine ililala bao 1-0 likifungwa na Paul Nonga, huku wao wakikosa penalti kupitia kwa nyota wake wa zamani, Chris Mugalu aliyegongesha mpira kwenye nguzo na leo inaondoka na pointi moja.

Bao la Seif linafika la tano kwake hadi sasa huku Awadh Juma akifikisha asisti ya tatu kwa Mbeya City na kuendelea kutengeneza uhusiano mzuri baina yake na Straika huyo sambamba na Sabilo.

Simba imewapumzisha Bocco, Okrah na Phiri na kuwaingiza Kibu Denis, Kyombo na Sakho. huku City wakimtoa Ngy'ondya na kumwingiza Gasper Mwaipasi.

Hii ni sare ya nne kwa Simba msimu huu huku ikiwa sare ya nne mfululizo kwa Mbeya City katika uwanja wa nyumbani kwani mara ya mwisho ilishinda 2-1 dhidi ya Namungo FC Novemba 11

Katika michezo 19 walizokutana tangu msimu wa mwaka 2013/14 City ikipanda Ligi Kuu, Simba imeshinda michezo 12, sare nne huku Mbeya City ikishinda michezo mitatu na walipokutana msimu uliopita uwanja huu City ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Paul Nonga.

Timu zote mbili mara ya mwisho kupoteza ilikuwa dhidi ya Azam, Mbeya City ikipoteza kwa bao lililofungwa na Idrisa Mbombo Uwanja wa Sokoine huku Simba ikilala kwa bao la Prince Dube Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Makocha wote walioziongoza timu hizo katika mchezo wa leo, hawakuwepo msimu uliopita, Simba ilikuwa na Pablo Franco na sasa, Juma Mgunda huku kocha wa Mbeya City alikuwa Mathias Lule na sasa, Abdalah Mubiru ambaye msimu uliopita alikuwa Gor Mahia ya Kenya.

John Bocco katika  minne iliyopita ameifunga Mbeya City mabao manne, akifunga mawili msimu wa mwaka 2019/20 na mawili 2020/21.

Mchezo uliozaa mabao mengi zaidi wakati timu hizo zikikutana ilikua Novemba 3, 2019 Simba ilishinda mabao 4-0 na Juni 22, 2021 ilishinda 4-1 michezo yote ikipigwa Uwanja wa Taifa (sasa Benjamin Mkapa).

Simba imefikisha pointi 28 ikiwa nafasi ya tatu huku Mbeya City ikiwa nafasi ya sita na pointi 19.