Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba yaendeleza ubabe kwa Yanga, yarudi kileleni

Muktasari:

  • Yanga Princess imewahi kupata ushindi mara moja tu dhidi ya Simba Queens kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.

Dar es Salaam. Simba Queens imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya mtani wake wa jadi, Yanga Princess kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake katika Uwanja wa KMC Complex leo.

Ushindi huo uliofanya Simba Queens kufikisha pointi 12, ulitokana na bao pekee la kujifunga la Danai Bhobho katika dakika ya 48 alipokuwa katika harakati za kuokoa krosi ya Elizabeth Wambui.

Wambui ambaye ameonyesha kiwango bora katika mchezo wa leo akishambulia na kuilinda vyema safu ya ulinzi ya timu yake, alimzidi kasi beki Chinemerem Angela wa Yanga Princess walipokuwa wakiwania pasi ya Precious Onyinyechi na kupiga pasi hiyo ambayo Bhobho alishindwa kuiokoa na kuijaza katika wavu wake, kuiandikia Simba bao pekee katika mechi hiyo.

Ni mchezo ambao ulikuwa wa kupishana baina ya timu hizo mbili ambapo nyakati kadhaa zilishambuliana kwa zamu katika nyakati kadhaa lakini safu zao za kushambulia hazikuwa makini kutumbukiza mpira wavuni.

Matokeo hayo yameifanya Yanga Princess kubakia katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi zake tatu ambazo ni tisa pungufu ya zile za vinara Simba Queens.

Kwa upande mwingine ushindi wa Simba Queens umeifanya ilipe kisasi cha kufungwa kwa mikwaju ya penalti 4-3 na Yanga katika mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii kwa wanawake msimu huu iliyochezwa mwezi uliopita.

Kocha wa Simba Queens, Yussif Basigi alisema kuwa amefurahishwa na ushindi wa timu yake leo.

"Ni mechi yangu ya kwanza dhidi ya Yanga hivyo ni furaha kuona kwamba tumepata ushindi na tunaendelea kuongoza msimamo wa ligi," alisema Basigi.

Edna Lema ambaye ni kocha wa Yanga Princess alisema kuwa timu yake ilicheza vyema ingawa imepoteza mchezo.

"Kuna udhaifu ambao tunao ninaomini tutaurekebisha lakini kwa namna tulivyocheza, matokeo ya sare yangekuwa ni sawa zaidi," alisema Edna.

Kikosi cha Yanga kilianza na Rita Akarekor, Danai Bhobho, Chinemerem Angela, Neema Paul, Asha Omary, Diana Antwi, Arier Odong, Agnes Pallangyo, Anastazia Lucia, Uzoamaka Confidence na Wema Richard.

Simba walianzisha kikosi kilichokuwa na Janeth Shija, Violeth Nicholaus, Dotto Evarist, Elizabeth Wambui, Fatuma Issa, Precious Onyinyechi, Vivian Corazone, Ruth Ingosi, Esther Erastus, Asha Djafar na Jentrix Shikangwa.