Simba yaikalia kooni Yanga

Mmoja wa mashabiki wa Simba akiwa na kichwa cha mbuzi na wengine wakishangilia baada ya mechi kati ya Simba na Tanzania Prison, kumalizika katika Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya jana na Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0. Picha na Godfrey Kahango.

Muktasari:

Baada ya kumalizana na Coastal Union, Simba itacheza na Kagera Sugar Mei 10 na Mei 13 itaivaa Azam kabla ya kupepetana na Mtibwa Sugar Mei 16 na itamaliza Dar es Salaam dhidi ya Ndanda Mei 19.

Dar es Salaam. Simba imezidi kupunguza pengo la idadi ya pointi baina yake na Yanga ambao wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya jana kupata pointi tatu dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Bao la mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi alilofunga dakika ya 11, baada ya uzembe wa mabeki wa Prisons kushindwa kuondoa mpira mrefu ambao mfungaji alimpiga chenga kipa Aaron Kalambo kabla ya kuweka mpira huo wavuni.

Okwi amefikisha mabao 11 katika ligi hiyo msimu huu, akiwa na kumbukumbu ya kufunga mabao 20 msimu uliopita.

Simba imefikisha pointi 78 baada ya kucheza mechi 30 na ipo nafasi ya pili, huku Yanga ambayo leo itacheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Lipuli inaongoza kwa pointi 80.

Yanga iko mbele kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Simba ikiwa imecheza mechi 34. Ushindi wa Simba unaongeza presha katika mbio za kuwania ubingwa dhidi ya kwa Yanga.

Timu hiyo Alhamisi itacheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Biashara United ugenini mkoani Mara wakati Simba itavaana na Coastal Union Jumatano, Dar es Salaam.

Endapo Simba itaifunga Coastal Union itafikisha pointi 81 ambazo zitakuwa tatu nyuma ya Yanga na kushika usukani wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu.

Mbali na Simba kuvuna pointi tatu dhidi ya Prisons, nyota wake Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, John Bocco, Clatous Chama na Adam Salamba wamekuwa hatari kuliko timu yoyote kwenye ligi.

Kagere anaongoza kwa mabao 17, Bocco (14), Okwi (11), Chama na Salamba kila mmoja amefunga manne.

Bao la Okwi alilofunga jana linawafanya washambuliaji watano wa Simba kufikisha idadi ya mabao 50. Simba imefunga mabao 61.

Baada ya kumalizana na Coastal Union, Simba itacheza na Kagera Sugar Mei 10 na Mei 13 itaivaa Azam kabla ya kupepetana na Mtibwa Sugar Mei 16 na itamaliza Dar es Salaam dhidi ya Ndanda Mei 19.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza Simba iliichapa Prisons bao 1-0, lililofungwa na Kagere, lakini msimu uliopita kwenye Uwanja wa Sokoine ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Bocco. Prisons imebaki nafasi ya tisa ikiwa imecheza mechi 34 na pointi 42.

Prisons: Aaron Kalambo, Michael Mpesa, Leons Mutelemwa, Nurdin Chona, Vedastus Mwihambi, Jumanne Nimkaza, Salum Kimenya, Ezekiel Mwashilindi, Adam Adam Ramadhani Ibata na Ismail Kada.

Simba: Aishi Manula, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni Yusuph Mlipili, James Kotei, Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere Emmanuel Okwi/Jonas Mkude na Haruna Niyonzima/Hassani Dilunga.