Simba yakomaa na Kapombe
Simba imekaa meza kufanya mazungumzo mapya na beki aliyemaliza mkataba wake, Shomari Kapombe ili kuendelea kuwepo katika kikosi hicho msimu ujao kama ripoti ya kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids inavyotaka.
Chanzo cha ndani kinasema baada ya kuondoka kwa aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho, Mohamed Hussein 'Tshabalala' aliyesaini mkataba wa miaka miwili Yanga, uongozi hautaki kumpoteza Kapombe atakayebakia kama mchezaji mwandamizi ndani ya kikosi.
"Mazungumzo ya kumuongezea Kapombe mkataba wa miaka miwili yameanza kufanyika na yana muelekeo mzuri, kwa asilimia kubwa tunaamini ataendelea kuwa sehemu ya kikosi kama ripoti ya kocha Fadlu ilivyotaka," kilisema chanzo hicho na kuongeza;
"Kapombe ameitumikia Simba kwa mafanikio kwa muda mrefu tunamchukulia kama mchezaji kiongozi dhidi ya wengine na ikiwezekana kwa baadaye aje kuinufaisha zaidi Simba kama ilivyokuwa kwa kina Mussa Mgosi ni kocha wa Simba Queens, Selemani Matola amekuwa kocha msaidizi wa muda mrefu wa Simba."
Msimu uliyopita Kapombe alifunga mabao matatu, asisti tatu, msimu wa nyuma yake 2023/24 alimaliza na asisti nne pia aliwahi kuwa MVP wa Ligi Kuu mwaka 2016.
Mbali na hilo msimu wa 2015/16 Kapombe aliweka rekodi ya kufunga mabao manane Ligi Kuu, akifunga moja Azam FC ikishinda mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union, dhidi ya Ndanda FC bao 0-1, dhidi ya Toto Africans mabao mawili Azam ikishinda mabao 5-0, dhidi ya Mgambo Shooting 2-0 dhidi ya Stand United bao 0-1 dhidi ya Kagera moja Azam ikishinda mabao 2-0.
WADAU
Kuhusiana na maamuzi ya Simba kumbakiza Kapombe, staa wa zamani wa timu hiyo Amir Maftah alisema:"Kikosi kinapokuwa na wachezaji wapya na waandamizi kinakuwa imara zaidi, Kapombe kaitumikia Simba kwa muda mrefu, hivyo anaweza akawa kiongozi mzuri dhidi ya wengine.
Mchezaji mwingine wa zamani wa klabu hiyo, Frank Kasanga 'Bwalya' alisema:"Simba wakimbakiza Kapombe watakuwa wamefanya kitu sahihi,baada ya kuondoka kwa Tshabalala lazima abakie kama mchezaji mwandamizi."