SIO ZENGWE: Kulalamika serikalini ni kusababisha taharuki?

SIO ZENGWE: Kulalamika serikalini ni kusababisha taharuki?

WAKATI Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka (TFF) ilipomtia hatiani makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kwa kosa la uchochezi, nilihoji jinsi chombo hicho kilivyoweza kufikia uamuzi huo mgumu kuuthibitisha.

Ni ushahidi upi ambao Kamati ya Maadili ingeweza kukubaliana nao kuwa Mwakalebela alifanya uchochezi, ambao hata huku katika mahakama za kawaida umekuwa ni mgumu kuthibitishwa ukirejea hukumu zilizowahi kutolewa dhidi ya kosa hilo.

Niliingiwa na wasiwasi kuwa kama uamuzi unaweza kufikiwa kwa njia hiyo, basi kuna uwezekano mkubwa wa chombo hicho kuonea wadau wengi wa soka kwa kosa hilo la kuchonga.

Ni kweli baadaye Mwakalebela aliomba radhi na kuondolewa adhabu, lakini angeweza kukomaa nayo hadi kubatilishwa kama kweli aliamini kuwa hakufanya uchochezi.

Maneno dhidi ya chombo fulani pekee hayawezi kutafsiriwa kuwa ni uchochezi hadi hapo itakapothibitika kuwa maneno hayo yaliamsha hisia fulani kwa kundi la watu fulani na wakapanga kufanya au wakafanya jambo kutokana na maneno hayo. Lakini kufikiri tu kuwa maneno hayo yanaweza kuchochea watu, hakuwezi kuthibitisha kuwa ni ya uchochezi.

Fikra zangu zilikuwa ni sahihi. Wiki kadhaa baadaye, TFF ikatangaza kuwa kijana mmoja ambaye ni mdau wa soka, akijihusisha zaidi na ukocha, amepatikana na hatia ya kosa la uchochezi na hivyo amefungiwa maisha kujihusisha na soka!

Kijana huyo, Liston Katabazi alitangazwa kufungiwa maisha kujihusisha na soka ndani na nje ya nchi Juni 24, 2021 kwa kosa la kutoa shutuma za uongo dhidi ya TFF ambazo alishindwa kuzithibitisha.

Kwanza ukiangalia kosa lenyewe “kutoa shutuma za uongo dhidi ya TFF” linastahili adhabu ya kufungiwa “maisha” kujihusisha na soka? Lakini ukiangalia katika mashtaka yake, ni kwamba alishtakiwa kwa kosa la kusababisha taharuki kwa umma siku ambayo alikwenda ofisi ya msajili wa vyama vya michezo wa wilaya ya Ubungo kupinga uchaguzi wa viongozi wa soka, akidai kuwa baadhi ya klabu zilizoshiriki kupiga kura hazijasajiliwa na ofisi hiyo na hivyo kutaka zienguliwe.

Tafsiri ya taharuki katika madai hayo ni ipi? Kwamba kwenda ofisi ya serikali kupinga taasisi inayohusishwa kwenye uchaguzi bila ya kusajiliwa na serikali ni kusababisha taharuki? Kwamba kwenda ofisi ya serikali ni kosa kubwa kwa mchezo wa mpira wa miguu?

Kwamba katika ofisi ya serikali kuna mikusanyiko mikubwa kiasi kwamba mtu akienda tu kulalamikia jambo fulani kuwa haliendeshwi kwa kufuata sheria za nchi, basi ni kusababisha taharuki kwa umma unaoshinda ofisi za serikali?

Lakini nyuma ya sakata hilo kunaweza kuwa na mambo mengi, labda dhidi ya viongozi, ambayo yalisababisha kutafutwa njia za kumdhibiti milele, bila ya kujali kwamba mlengwa aliamua kuwa mpira ndio uwe maisha yake. Inakuwaje wale ambao mpira si maisha yao, waamue hatima ya huyu ambaye amewekeza nguvu zake kuendesha maisha kwa kutumia mpira?

Ni dhahiri kuwa huyu kijana Katabazi ameonewa kwa kiwango kikubwa ambacho hakustahili. Kuikosoa TFF si tatizo na kizuri zaidi ni kwamba hakulalamika vichochoroni, bali alitumia mamlaka zilizowekwa na serikali kuhoji uhalali wa hatua fulani ambazo anahisi hazifuati sheria za nchi. Jibu lilikuwa ni kuthibitisha kuwa hizo klabu alizolalamikia zina usajili halali wa serikali na si kukimbilia kumfungia MILELE eti kwa sababu ya kuhoji uhalali.

Ni muhimu kwa kamati ya maadili kufanya kazi zake kwa kuheshimu misingi ya haki na kutoa adhabu kulingana na ukubwa wa kosa na si kutoa adhabu ambazo zinalenga kumkomoa mshtakiwa au kumzuia kabisa kujihusisha na mchezo alioamua kuutumikia badala ya kumtengenezea mazingira ya kujifunza au kujirekebisha kama kweli amekosea.

Adhabu kama hizo hazijengi mpira na badala yake zinajenga ‘chawa’ ambao daima watakuwa wanasifia wakati mambo yakiharibika. Tunahitaji kurudi kwenye akili zetu badala ya kufanya mambo kwa njia ambazo zitarudisha nyuma watu wenye akili tofauti ambayo ni muhimu katika maendeleo ya kila kitu.