SIO ZENGWE: Mbinu mpya za uchaguzi CAF zinavutia

Uchaguzi wowote wa kupata viongozi wa michezo, hasa mpira wa miguu hutawaliwa na mbinu chafu za kila aina, kudhalilishana, habari za kupotosha, kubambikiana kashfa na huishia kwa wapiga kura kuwa na mgawanyiko ambao huchukua muda kuumaliza.

Kama huoni mambo hayo, ujue mmoja wa wagombea ana nguvu zisizo kifani na hivyo kunakuwa hakuna hata haja ya kutengezeana zengwe kwa kuwa ushindi ni bayana.

Na kama anayegombea ni kiongozi aliye madarakani, huwa katika mazingira kama hayo ya kutokuwa na mpinzani mkubwa kwa sababu atakuwa ama amewamaliza kwa kutumia vyombo huru kuwaadhibu ama kutumia vibaya madaraka kuwapumbaza wapigakura kama ilivyokuwa kwa mgombea wa sasa wa urais wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), Ahmad Ahmad, ambaye alidiriki hata kubadilisha mfumo wa kufuzu kwa fainali za michuano ya umri ili kutoa kile anachokiita ‘nafasi sawa’ kwa kila kanda kushiriki michuano ya fainali za U-17 na U-20 au michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN).

Lakini hali ni tofauti wakati huu wa kuelekea uchaguzi wa rais wa CAF uliopangwa kufanyika Machi 12 jijini Rabat, Morocco.

Ingawa uchaguzi huu ulitanguliwa na matukio kama Ahmad kufungiwa kwa muda mrefu na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kutokana na tuhuma kadhaa za matumizi mabaya ya madaraka na rushwa, hali inaonekana kuwa tulivu baada ya rais wa soka nchini Morocco kufanya jitihada binafsi za kukutanisha wagombea na kuwaeleza hoja kubwa ya Waafrika kwa sasa katika soka badala ya vita ya uchaguzi ambayo huisha kwa mgawanyiko.

Fouzi Lekjaa, rais wa Chama cha Soka cha Morocco (FRMF) aliwaalika wagombea wane wa urais wa CAF na kuwashauri kuahiri umoja badala kuzidisha mgawanyiko unaotokana na uchaguzi, jambo ambalo rais wa Fifa, Gianni Infantino pia amekuwa akisisitiza katika ziara zake barani Afrika, akifahamu fika kuwa rais wa CAF ndiye naibu rais wa Fifa.

Mbali na Ahmad, ambaye anatokea Madagascar, wagombea wengine wa urais ni Jacque Anouma, kiongozi veteran katika soka na rais wa zamani wa Chama cha Soka cha Ivory Coast, Patrice Motsepe, mfanyabiashara Tajiri barani Afrika na mmiliki wa klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Augustin Senghor wa Senegal.

Habari zinasema kuwa kikao hicho kimeishia kwa wane hao kukubaliana kujiondoa ili kumpisha Motsepe awe rais, wakati Senghor na Yahya watakuwa manaibu wake huku Anouma, ambaye pia alikuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Fifa, akiwa mshauri wake.

Suala hilo linaweza kumalizwa leo Jumatatu huku shauri la Ahmad likisubiriwa kumalizika na hivyo uchaguzi kufanyika kwa ajili ya kufanya mageuzi katika uendeshaji soka baada ya utawala wa Ahmad kutuhumiwa kufuja akiba aliyoiacha Issa Hayatou na kutokuwa na dira imara.

Tayari Motsepe ameshaeleza ilani yake na ameahidi kutumia uzoefu wake katika biashara kushawishi kampuni kubwa duniani kuwekeza katika soka Afrika. Staili ya kampeni katika uchaguzi huu kama itafanikiwa, maana yake Afrika itakuwa imepata njia mpya ya kuondokana na chaguzi zinazoishia katika kuvuruga vyama au klabu.

Mara nyingi taasisi zinakwenda katika uchaguzi zikiwa hazijui hoja kuu inayozikabili na hivyo kwenda kuchagua mtu ambaye ana uwezo wa kifedha bila ya kuwa na dira, au mtu ambaye alifanya kampeni zake vizuri.

Kila uchaguzi unapokaribia ni lazima kujua uongozi unaomaliza umefanya nini na nini kinatakiwa kifanywe na viongozi wanaokuja na ndio maana imekuwa rais kwa wagombea hao wane kufikia muafaka na kukubaliana nini cha kufanya. Hizi ndizo siasa zinazotakiwa. Pamoja na ukweli kwamba demokrasia ni lazima itawale katika uchaguzi, lakini kujua unataka nini katika uchaguzi kabla ya kufanya uamuzi ni muhimu sana.