SIO ZENGWE: Tumekimbilia kuishinda Simba kwa kura ishu ya GSM

Muktasari:

  • Real Madrid, Barcelona na Athletic Bilbao zimekataa kuidhinisha mpango uliopendekezwa na Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) wa kuuza asilimia 11 ya mapato yao kwa kampuni ya uwekezaji ya Marekani inayoitwa CVC kwa miaka 50 ijayo.

Real Madrid, Barcelona na Athletic Bilbao zimekataa kuidhinisha mpango uliopendekezwa na Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) wa kuuza asilimia 11 ya mapato yao kwa kampuni ya uwekezaji ya Marekani inayoitwa CVC kwa miaka 50 ijayo.

Klabu hizo kubwa tatu, na UD Ibiza na ambazo zinaungwa mkono na Shirikisho la Soka la Hispania, zinadai kuwa kukubaliana na mpango huo ni kuweka rehani hali ya baadaye ya klabu hizo na kwamba mpango huo, si tu unakiuka kanuni za msingi za sheria za michezo nchini Hispania, bali pia katiba ya La Liga.

Mpango huo ulipitishwa na klabu 37 kati ya 42 zinazoshiriki La Liga na ligi daraja la pili, huku klabu moja ambayo haijajulikana ikiamua kutopiga kura.

Mbali na hoja hizo, klabu hizo tatu pia zinadai kuwa La Liga imetumia kipindi hiki cha kuyumba kiuchumi kwa klabu za barani Ulaya, kupitisha mpango huo ambao utazipatia klabu zilizoidhinisha mgawo wa awali wa Euro 400 milioni chini ya mpango huo unaoitwa Project Impulse.

Lakini klabu hizo tatu hazikuwa mikono mitupu wakati wa kupinga mradi huo. Zilijaribu kuziandikia klabu nyingine kuzielewesha kuhusu athari za Project Impulse na kupendekeza mradi mwingine wa Project Sustainable ambao unaungwa mkono na JP Morgan, Benki ya Amerika na ya HSBC, moja ya benki kubwa duniani.

Zinasema mpango huo ambao pia ni wa Euro 2 bilioni wa miaka 25 na wa riba ya kiwango cha asilimia 2.5 hadi 3, ni wa muda mrefu, endelevu, wa haki na wa kisheria na utakuwa bora mara 15 zaidi ya huo wa CVC.

Nimetanguliza muhtasari huo kuonyesha mambo mengi. Kwamba, kumbe Shirikisho la Soka la Hispania linapingana na La Liga kuhusu mpango huo wa kuuza asilimia 11 ya mapato ya haki za TV kwa miaka 50? Kwamba kumbe suala la uuzaji wa haki hizo, si tu unazihusu klabu za La Liga, bali hata za Ligi Daraja la Pili ambazo ni wanahisa wa La Liga?

Kwamba kumbe kampuni kubwa zinaweza kutumia hali ya kuyumba kiuchumi kuweka mezani dau ambalo linaweza kukubalika bila ya kuruhusu akili kufanya kazi hata kidogo? Kwamba kumbe ukipinga mradi fulani ni muhimu kuwa na mbadala? Kwamba, ili kupitisha, klabu zinakuwa na ufahamu mkubwa wa pendekezo la mradi?

Kwa namna moja au nyingine, sakata hilo la Hispania ambalo sasa limefika mahakamani, lina uhusiano fulani na sakata la udhamini uliosababisha utata wa kampuni ya GSM kwenye Ligi Kuu.

Kwa kutofikiria kwa kina, unaweza kuibuka na jibu jepesi tu kwamba “cha msingi ni fedha” na si kujua kwa kina na mapana kuhusu mkataba unaowasilishwa kwa klabu za Ligi Kuu, na kwa maana nyingine za Ligi Daraja la Kwanza, ambazo zinatakiwa kuwa na hisa katika Bodi ya Ligi, kwa kuwa hata kama mkataba unahusu udhamini wa Ligi Kuu pekee, ni lazima kwa kiasi fulani unufaishe ligi ya chini yake ambayo huingiza timu Ligi Kuu. Sitazungumzia ni kwa jinsi gani, lakini akili ya haraka inaona hilo.

Simba, ambayo ilipiga kura ya kupinga mradi huo, si kwamba haitaki GSM idhamini Ligi Kuu, bali inaona utata ambao ni muhimu kutolewa maelezo ya kina kabla ya kuidhinishwa. Ni wazi kuwa ushiriki wa baadhi ya wafanyakazi wa GSM katika uendeshaji wa klabu ya Yanga na pia udhamini wa ligi nzima, lazima uitishe Simba. Na hofu hiyo ni dhahiri, hata kama wahusika hawatashiriki katika vitendo ambavyo Simba wanaona vinaweza kuathiri mpira na matokeo yake.

Ni lazima kuwe na mipaka kati ya watendaji wanaohusika na usimamizi wa udhamini wa Ligi Kuu na wale wanaohusika na udhamini wa klabu, angalau ile hofu itapungua.

Lakini GSM ni mdhamini wa jezi wa Yanga, wakati mdhamini kama huyo kwa Simba ni Vunja Bei, ambaye ana haki peke (exclusive rights) Simba. Yaani Simba ikija na mdhamini mwingine ambaye ni benki, TFF au Bodi ya Ligi zitakuwa tayari kuiachia iweke nembo yake kwenye jezi zake huku NBC ikiwa bega moja?

Hebu angalia! Ile VVIP ilishikwa na TFF siku ya mechi ya Simba v Yanga na wenyeji Simba kualikwa, mabega yote mawili sasa yamechukuliwa na TFF au Bodi ya Ligi, fursa kwa klabu kutengeneza fedha zake binafsi ziko wapi?

Kuna hoja nyingi ambazo zinahitaji mijadala ya kina ili kufikia uamuzi ambao utafungua macho zaidi klabu kujua fursa zilizopo katika kushiriki Ligi Kuu badala ya kusubiri kuletewa chakula katika sahani ya dhahabu.

Real Madrid na Barcelona ni klabu kubwa ambazo zinaelewa fursa na nguvu yao ya kuvuta fedha nyingi zaidi ya zile zinazoweza kuwekwa mezani na La Liga. Tunaiangaliaje Simba katika kutaka maelezo ya kina ya udhamini wa GSM?

Au tunakimbilia kupiga kura kuonyesha wengi ndio waliopitisha na si kile kinachoelezwa na Simba. Tunahitaji kutoka huko.