Uholanzi, England nusu fainali ya nani zaidi
Muktasari:
- England na Uholanzi wanacheza nusu fainali ya pili kila mmoja akisaka nafasi ya kucheza fainali dhidi ya Uhispania.
Dortmund,Ujerumani. Kwa mara ya pili ndani ya miaka mitano, England na Uholanzi zinakutana kwenye hatua ya nusu fainali awamu hii ikiwa ni katika mashindano ya mataifa ya Ulaya, Ujerumani leo huku lengo likiwa ni moja tu ambalo ni kutinga fainali.
Kipute hicho kitaanza kupigwa kuanzia saa 4:00 usiku, muda wa Afrika Mashariki na kitafanyika katika Uwanja wa BVB uliopo Dortmund.
Mechi hiyo ya leo inakumbushia mchezo wa nusu fainali ya mashindano ya Ligi ya Mataifa ya Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (Uefa Nations League) 2019 ambao Uholanzi iliibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Uholanzi ilitinga hatua ya nusu fainali baada ya kuichapa Uturuki kwa mabao 2-1 kwenye hatua iliyopita wakati England ilipata tiketi ya kucheza nusu fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti 5-3 mbele ya Switzerland baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika dakika 120.
Mzani uko sawa
Mshindi wa mchezo wa leo atakuwa mbabe rasmi wa mwenzake kutokana na matokeo ya mechi za nyuma za kimashindano baina ya timu hizo kuwa sare.
Katika mechi 23 za mashindano tofauti ambazo timu hizo zimewahi kukutana, kila moja imeibuka na ushindi mara saba na zimetoka sare tisa.
Timu hizo zinakaribia pia kufanana katika matokeo ya mechi tano zilizopita ambazo kila moja imecheza ambapo Uholanzi imepata ushindi mara tatu, kupoteza moja na kutoka sare moja wakati huo England ikipata ushindi mara tatu na kutoka sare mbili.
Kumbukumbu zinaonyesha katika mechi tisa zilizopita ambazo timu hizo zimekutana, England wamepata ushindi mara moja tu, sare nne na kupoteza mechi nne.
Mechi ya kujuana
Ni mchezo ambao unatarajia kukutanisha wachezaji 13 kati ya 22 wwnaotegemewa kuanza ambao wanafahamiana kutokana na kucheza pamoja katika Ligi Kuu ya England (EPL).
Nyota tisa kati ya 11 wanaotegemewa kuanza kwenye kikosi cha England wanacheza EPL kama ilivyo kwa nyota wanne wanaotegemewa kuanza katika kikosi cha Uholanzi.
Wachezaji 10 wa England wanaocheza EPL ni Jordan Pickford, Kyle Walker, John Stones, Marc Guehi, Bukayo Saka, Kobie Mainoo, Declan Rice, Luke Shaw na Phil Foden.
Ni nyota wawili tu katika kikosi cha England kinachotegemewa kuanza leo ambao hawachezi katika klabu za nyumbani ambao ni Harry Kane (Bayern Munich) na Jude Bellingham (Real Madrid).
Kwa upande wa Uholanzi, nyota wake wanne ambao wanacheza EPL ni Bart Verbruggen, Virgil van Dijk, Nathan Ake na Cody Gapko.
Wengine saba wanaounda kikosi wanacheza ligi tofauti na EPL ambao ni Stefan de Vrij, Xavi Simons, Memphis Depay, Tijjani Reijnders, Donyell Malen, Denzel Dumfries na Jerdy Schouten.
Wajerumani kubeba lawama
Marefa kutoka Ujerumani ndio wamepangwa kuchezesha mechi hiyo wakiongozwa na mwamuzi wa kati, Felix Zwayer ambaye aliwahi kutuhumiwa kwa upangaji wa matokeo miaka ya nyuma.
Zwayer (43), aliwahi kufungiwa miezi sita baada ya kubainika alipokea kiasi cha Euro 300 ikiwa ni hongo kutoka kwa refa mwenzake Robert Hoyzer mwak 2005.
Uamuzi wa kumteua Zwayer kuchezesha mechi hiyo umeonekana kuzua mijadala kwa vyombo vingi vya habari na mashabiki wa soka ambao wanaamini kwamba fursa hiyo ilitakiwa kwenda kwa refa mwingine.
Hata hivyo kamati ya nidhamu na maadili ya Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (Uefa) ilishikilia msimamo wake wa kumteua Zwayer kuchezesha mchezo huo.
Zwayer amekuwa ni refa wa bahati nzuri kwa England kwani imepata ushindi katika mechi zote tatu za hapo nyuma ambazo amewahi kuichezesha wakati kwa Uholanzi imepata ushindi mara moja tu katika mechi tatu huku ikipoteza mbili.
Refa msaidizi namba moja kesho atakuwa ni Stefan Lupp, Marco Achmuller akiwa msaidizi namba mbili na refa wa nne akipangwa Daniel Siebert wakati mwamuzi atakayekuwa katika teknolojia ya video ya usaidizi kwa marefa (VAR) akiwa ni Bastian Dankert.