USAJILI: Simba SC yasajili beki wa Lipuli

‘Lengo letu ni kuhakikikisha tunafanya usajili makini ambao utaifanya Simba ifanye vizuri msimu ujao.’
Hanspope
Muktasari:
- Ni beki aliyeibuliwa kupitia mpango wa maboresho ya Taifa Stars aliyekuwa akiwaniwa na Yanga.
Dar es Salaam. Simba imemsajili beki wa Lipuli na Taifa Stars, Joram Mgeveke kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mgeveke aliyeibuliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia mpango wake wa maboresho ya Taifa Stars, alisaini mkataba wa miaka mitatu wa kuichezea Simba jana mjini Iringa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe akizungumza jana akiwa safarini kutoka Iringa kuja Dar es Salaam alisema klabu yake imemalizana na Mgeveke na sasa ni mchezaji halali wa Simba.
“Tumemsajili yule beki chipukizi wa Taifa Stars anayefahamika kwa jina la Joram kwa mkataba wa miaka mitatu na kazi hiyo imefanyika leo (jana) mjini Iringa.
“Kazi ndiyo tumeianza kwa kumsajili Joram na tutaendelea kuwasajili wengine kwa kuzingatia mapendekezo ya benchi la ufundi,” alisema Hanspope.
Aliongeza: “Lengo letu ni kuhakikikisha tunafanya usajili makini ambao utaifanya Simba ifanye vizuri msimu ujao wa ligi na kurejea kwenye hadhi yake.”
Kwa upande wake, Mgeveke alipotafutwa alikiri kumalizana na Simba kwa kujiunga nayo kwa mkataba wa miaka mitatu.
“Kifupi nimemalizana na Simba na kimsingi nimefurahi kwa vile ni hatua nyingine ya maisha yangu ya soka ukizingatia Simba ni timu kubwa hapa Tanzania.
“Jambo la muhimu lililobaki kwangu ni kuongeza juhudi katika mazoezi ili niweze kupata namba ya kudumu,” alisema Mgeveke.
Kitendo cha Simba kumnasa Mgeveke kinaweza kutafsiriwa ni pigo kwa wapinzani wa timu hiyo Yanga ambayo pia ilikuwa katika mipango ya kumsajili beki huyo.
Simba sasa ipo katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wao wapya huku wakitarajia kufanya uchaguzi huo Juni 29, ili uongozi mpya ukabidhiwe jukumu la kufanya usajili.
Simba inaingia katika uchaguzi mkuu ikiwa na kumbukumbu ya kufanya vibaya misimu miwili iliyopita ya Ligi Kuu Bara na kukosa nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwani kwa misimu hiyo miwili licha ya kukosa ubingwa, Simba imeshindwa hata kukamata nafasi ya pili.
Klabu hii kongwe inaangalia zaidi uchaguzi huu na kuuhusisha na mafanikio ya timu yao uwanjani kwani viongozi watakaowachagua watakaa madarakani kwa miaka minne ijayo.