Yanga hii haiachi mtu, yaichapa Lyon 3-0

Yanga hii haiachi mtu, yaichapa Lyon 3-0

Muktasari:

  • YANGA imeiva kuivaa KMC Jumamosi ya wiki hii katika muendelezo wa mechi za Ligi Kuu baada ya kumalizika kwa siku 21 za maombolezo ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati John Pombe Magufuli.

YANGA imeiva kuivaa KMC Jumamosi ya wiki hii katika muendelezo wa mechi za Ligi Kuu baada ya kumalizika kwa siku 21 za maombolezo ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hayati John Pombe Magufuli.

Kutokana na kiwango walichokionyesha katika mchezo wao wa kirafiki, leo jioni Yanga walionekana kuimarika katika kila idara, huku kila mchezaji akaonyesha uwezo wake.

Wachezaji wote walionekana kuwa na utimamu wa mwili, kwani benchi la ufundi lilitoa nafasi kwa kila mchezaji kucheza mechi hiyo.

Yanga imeshinda mabao 3-0, mechi iliyopigwa Uwanja wa Avic Town uliopo Kigamboni jiji Dar es Salaam, mabao hayo yalifungwa, Micheal Sarpong dakika ya 12, Fiston kwa Penalti dakika ya 20 baada ya Feisali Salum kuchezewa rafu na Paul Godfrey 'Boxer dakika ya 90 kwa shuti la mbali.

Japokuwa Lyon imechapwa lakini mechi hiyo ilikuwa na ushindi wa juu.

Katika kikosi cha Lyon wamecheza wachezaji wa zamani wa timu ya Yanga ambao ni Jerry Tegete na Jofrey Mwashiuya.

Mashabiki wa Yanga, walifurika kuangalia mechi hiyo, ambapo walionyesha kufurahishwa na kiwango kilichoonyesha mastaa wao na kuamini KMC itachapwa.

Mwanaspoti limewasikia mashabiki hao wakisemezana kwamba kwa sasa hawana hofu Yanga ikicheza mechi yoyote kwa maana ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam.

"Hapa ni kazi tu, iwe ligi Kuu ama FA lazima tupate matokeo yakutupa kicheko,"wamesikika wakisemezana kwa kicheko.

Imeandaliwa na Olipa Assa, Thomas Ng'itu na Khatim Naheka