Yanga mitihani migumu Ghana

Dar es Salaam. Wakati kikosi cha Yanga kikiwasili jana Ghana kwa ajili ya kuikabili Medeama, keshokutwa Ijumaa, mambo manne yanailazimisha kuibuka na ushindi katika mechi hiyo itakayochezwa katika Uwanja wa Baba Yara, Kumasi kuanzia saa 1:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki.

Mchezo huo ni wa raundi ya tatu ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku ukizikutanisha timu hizo kwa mara ya tatu.

Jambo la kwanza linaloilazimisha Yanga kuibuka na ushindi ni kuweka hai matumaini yake ya kutinga hatua ya robo fainali na itafikisha pointi nne zinazoweza kuisogeza hadi nafasi ya tatu au ya pili kwenye kundi lake D kutokana na matokeo ya mechi baina ya Al Ahly na CR Belouizdad.

Kwa sasa Yanga ipo mkiani mwa kundi hilo na pointi yake moja ambayo imepata katika mechi mbili na ilianza kwa kupoteza kwa mabao 3-0 mbele ya Belouizdad na kisha kutoka sare ya bao 1-1 na Al Ahly.

Mtihani wa pili kwa Yanga ni kulipa kisasi cha mwaka 2016 na ilipoteza kwa mabao 3-1 mbele ya Medeama zilipokutana Ghana katika mechi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika huku mechi iliyochezwa hapa Dar es Salaam baina yao ikimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Kibarua cha tatu cha Yanga ni kumaliza rekodi ya ubabe nyumbani ya Medeama katika mashindano ya kimataifa na timu hiyo ya Ghana tangu ilipoanzishwa mwaka 2011 hadi sasa haijawahi kupoteza mechi yoyote nyumbani katika mashindano ya klabu Afrika.

Timu hiyo imecheza mechi 13 za mashindano ya klabu Afrika katika ardhi ya nyumbani, ikishinda 12 na kutoka sare moja, ikifunga mabao 27 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita.

Deni la nne kwa Yanga ni kumaliza unyonge ilionao katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo haijawahi kuonja ladha ya ushindi hadi sasa ikishiriki kwa mara ya pili.

Yanga ambayo mara yake ya kwanza kushiriki hatua hiyo ilikuwa ni 1998, imeshacheza mechi nane za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na imetoka sare nne na kupoteza mechi nne, ikifunga mabao sita na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 23.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema wanafahamu ugumu wa kukabiliana na Medeama ugenini hivyo wanajipanga kuhakikisha wanapata ushindi.

“Hakuna mechi rahisi, kila mchezo ni mgumu hasa unapocheza ugenini, tumekuwa na siku moja pekee ya maandalizi kuelekea mechi hii ya ugenini ila hii sio sababu tunatakiwa kupambana,” alisema Gamondi ambaye bado anausaka ushindi wa kwanza kwenye hatua ya makundi.

“Tunawaheshimu wapinzani wetu ni timu ambayo inaundwa na wachezaji bora, kwetu sisi hatuna nafasi ya kusema twende tukajilinde lakini kitu muhimu ni kucheza kwa nidhamu kubwa.

“Tukizuia vizuri na kisha kutumia nafasi za kufunga nafikiri tunaweza kupata matokeo tunayoyatafuta ni suala la kila mchezaji kutambua umuhimu wa ushindi kwa nafasi ambayo tupo sasa,” alisema Gamondi.