Yanga, Simba tatizo liko hapa
Dar es Salaam. Udhaifu unaokaribia kufanana unaonekana chanzo cha Yanga na Simba kushindwa kutamba katika mechi mbili za mwanzo za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo zilicheza nyumbani na ugenini katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
Takwimu za raundi mbili zilizopita za hatua ya makundi ya mashindano hayo zilizotolewa na mtandao wa www.fotmob.com zimeonyesha udhaifu wa Simba na Yanga katika kutengeneza nafasi za mabao, pia kushambulia kupitia krosi.
Katika utengenezaji wa nafasi kubwa ya bao, Simba na Yanga hadi sasa kila moja imefanya hivyo mara moja tu katika mechi mbili zilizopita tofauti na timu nyingine ambazo zimeonekana kuwa tishio katika kutengeneza nafasi kubwa za mabao.
Kinara wa kutengeneza nafasi kubwa za mabao ni Al Ahly ya Misri ambayo hadi sasa imefanya hivyo mara nane ikifuatiwa na Esperance na Pyramids FC ambazo kila moja imetengeneza nafasi kubwa za mabao tatu.
Timu hizo mbili zinazoiwakilisha Tanzania kwenye mashindano hayo, zinakabiliwa na changamoto ya upigaji mipira michache ya krosi kulinganisha na wapinzani wao wengine jambo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi na makocha wao wakati zikijiandaa na mechi za raundi ya tatu.
Wakati Yanga ikiwa na wastani wa kupiga krosi 3.5 kwa mchezo huku Simba yenyewe ikiwa na wastani wa kupiga krosi tatu kwa mechi, timu ya Wydad inaongoza ikiwa na wastani wa kupiga krosi nane (8) kwa mechi hadi sasa.
Asec Mimosas yenyewe inashika nafasi ya pili ikiwa na wastani wa krosi 6.5 kwa mechi huku Etoile du Sahel ikiwa nafasi ya tatu na wastani wa krosi 5.5.
Yanga na Simba zimeonekana pia kuwa na tatizo la kukosa shabaha pindi wanapokaribia lango la timu pinzani kutokana na kupiga idadi ndogo ya mashuti yaliyolenga lango kulinganisha na yale ambayo hayajalenga.
Katika mechi mbili ambazo Yanga imecheza dhidi ya CR Beloizdad na Al Ahly, imepiga mashuti 22 na kati ya hayo ni mashuti matano tu yaliyolenga lango huku moja likizaa bao na mengine manne yakishindwa kutoa matunda chanya.
Simba katika mechi zake mbili ilizocheza na Asec Mimosas na Jwaneng Galaxy, imepiga mashuti 23 na kati ya hayo, sita tu ndio yalilenga lango huku ikifunga bao moja na mashuti 17 yakishindwa kuipa faida.
Nyota wa zamani wa Taifa Stars, Mohammed Adolph ‘Rishard’ alisema Yanga na Simba zinapaswa kufanya tathmini ya kina ili zisifanye vibaya katika mechi zilizo mbele yao.
“Sio mwanzo mzuri kwa Simba na Yanga na ukiangalia namna timu nyingine zinavyocheza utaona kwamba mechi zilio mbele yao ni ngumu pengine kuliko hata hizo ambazo zimeshacheza.
“Kuna maeneo kama ya ushambuliaji na ulinzi zinaonekana haziko imara, sasa unapocheza mechi za aina hii ukikosea tu wapinzani wanakuadhibu,” alisema Rishard.