Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga: Okwi ni mali yetu

Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji (anayesoma karatasi) akiingia kwenye ukumbi wa mikutano wa klabu hiyo kwa ajili ya kuzungumza na waandishi wa habari jana kuhusu mchezaji Emmanuel Okwi aliyesajiliwa na Simba. Picha na Michael Matemanga.     

Muktasari:

Yanga ina mkataba wa miaka miwili na Okwi hivyo imeitaka TFF kuingilia kati suala la mchezaji huyo kusajiliwa Simba.

Dar es Salaam. Uongozi wa Yanga umewafungulia mashtaka katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mshambuliaji Emmanuel Okwi na uongozi wa Simba ukitaka ulipwe fidia ya dola 500,000 (Sh814,580,000) kwa mchezaji huyo kukiuka mkataba wa Yanga na kujiunga Simba.

Pia katika mashtaka hayo, Yanga inataka Okwi afungiwe kujishughulisha na masuala yote ya soka nchini Tanzania, pia Simba iadhibiwe kwa kufanya mazungumzo na mchezaji huyo kinyume cha kanuni za Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa) na wakala aliyehusika katika mazungumzo hayo afungiwe kujihusisha na shughuli za michezo nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji alisema Yanga bado ina mkataba wa miaka miwili na Okwi hivyo wameipa TFF siku saba kuhakikisha wanashughulikia mashtaka walioyapeleka dhidi ya Okwi.

“Ndani ya siku saba TFF isipotoa uamuzi wa suala hili tutaenda Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ikishindikana tutaenda Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa), fedha kwetu siyo tatizo, nilikuwa wa kwanza kuipongeza Simba ilipoifunga Yanga mabao matatu kwenye mechi ya mtani jembe, nikawa wa kwanza kuupongeza uongozi mpya wa Simba, nilidhani wamekuja watu ambao wanapenda kuendeleza mpira nchini, lakini kumbe wanataka vurugu.

“Mimi kama vurugu naziweza. Kama Simba wanataka hivyo sawa. Nimeamua tu kutulia, lakini nina uwezo wa kuwasajili wachezaji wote wa Simba kama TFF wataruhusu nikawalipa kila kitu kazi yao ikawa ni kufanya mazoezi pale Coco Beach kila siku basi. Uwezo huo ninao, mshahara wa wachezaji wa Simba kwa mwaka ni mshahara wa wachezaji wa Yanga kwa miezi miwili,” alisema Manji.

Alisema kwa sasa Yanga inachotaka ni kulipwa fidia ya dola 500,000 kwa vile Simba wamefanya makosa ya kumsajili na kumvalisha jezi Okwi wakati wakijua wazi ni mchezaji halali wa Yanga.

“Hiyo ndoa ni haramu kwa vile wameenda kinyume. Huwezi kusema mimi nina fedha za mafuta basi nasajili tu, kuna kanuni zipo wazi hata kuvunja ndoa kuna taratibu zake kwa mke na mume kabla ya kuachana na si kila mwanamke anayepita barabarani basi ni wa kuchukua, wengine wana wenyewe,” alisema Manji.

Naye Mwanasheria wa Okwi, Edgar Agaba ambaye pia ni wakala wa mchezaji huyo alipozungumza na gazeti hili kuhusiana na suala hilo alisema, “Yanga wasiniingize kwenye ugomvi wao, mimi hilo la Okwi kwenda Simba halinihusu wala silijui, Yanga wamalizane wenyewe na Simba, ukweli ulio wazi Okwi anaidai Yanga,” alisema Agaba.

Wakati Agaba akisema hayo, Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alisema TFF bado inatambua mkataba wa Okwi na Yanga na kwamba hakuna nyaraka yoyote ya kuvunja mkataba kati ya Yanga na Okwi.

“Hakuna nyaraka yoyote ya kuvunja mkataba. Tumeshawaandikia Yanga barua kuwaita kwenye shauri hili. Madai yaliyopo mpaka sasa ni Yanga kumlalamikia Okwi kushindwa kuripoti kwenye klabu yake, hakuna madai yoyote ya Okwi kuwa anaidai Yanga,” alisema Mwesigwa.

Simba SC ilimuuza Okwi mwaka 2013 katika klabu ya Etoile du Sahel na ilitaka kumrejesha kundini mwaka jana, lakini aliikwepa na kwenda SC Villa ya Uganda.

Okwi aliuzwa na Simba kwa Etoile kwa ada ya Dola 300,000, lakini Watunisia hao walishindwa kuwalipa Simba fedha za usajili huo kwa wakati, pia Okwi aligoma kuwachezea Waarabu hao kwa madai ya kushindwa kuheshimu makubaliano ya kimkataba.

Baada ya mgomo uliochukua miezi kadhaa SC Villa ambayo ndiyo iliyomkuza Okwi, iliomba Fifa, kumruhusu arudi Uganda ili asipoteze kiwango chake na Fifa ilimruhusu kwa kumpa kibali cha miezi sita wakati suala lake likitatuliwa hata hivyo alimwaga wino wa kuichezea Yanga kitu ambacho Simba wamedai kutumia mbinu hizohizo za Yanga kumrudisha Msimbazi.