Yanga Princess yapitisha panga mapema tu

UONGOZI wa klabu ya Yanga jana ulitangaza rasmi kuvunja mkataba na makocha wa timu ya Yanga Princess Edna Lema na Mohammed Hussein "Mmachinga".

Taarifa hiyo imekuja baada ya Yanga Princess kupoteza mchezo wa kwanza katika Ligi Kuu ya Wanawake wakipokea kichapo cha bao 1-0 na Fountain Gate Princess katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

"Uongozi umefikia makubaliano ya kuvunja mkataba kocha Mkuu wa Yanga Princess, Edna Lema na msaidizi wake Mohamed Husein "Mmachinga" kuanzia sasa," ilisema taarifa hiyo na kuongeza,

"Klabu inawashukuru na kuwatakia kila la heri katika majukumu mengine, klabu itatoa taarifa kuhusiana na mbadala wa nafasi hizo hivi karibuni." 

Kocha Edna ameandika kati ukurasa wake wa istagram na kusema hawezi kuwa adui wa klabu hiyo na kwake bado ni familia.

"Hatuwezi kuwa maadui kwa sababu mimi sio sehemu ya Yanga bado mtabaki kuwa familia yangu, viongozi pamoja na mashabiki niwashukuru tena na tena kwa mapenzi yenu kwangu najua kuna wanaonipenda sana lakini timu kwanza mtu badae,"ameandika Edna.

Ikumbukwe makocha Lema na Mmachinga wameitumikia Yanga Princess tangu timu imepanda Ligi Kuu msimu wa 2019/2020.

Katika msimu wa 2021/2022 kocha huyo aliweza kuifanikisha timu kumaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi 54, Fountain Gate Princess ya pili, wakati Simba Quens ikiibuka bingwa.

Timu hiyo ikiwa haina kocha mkuu wa kocha msaidizi inakutana Mkwawa Queens leo katka Uwanja wa Uhuru ikiwa ni raundi ya pili kwenye ligi liyoaanza Desemba 6.