Yanga, Simba kukutana Agosti 12 Ngao ya Jamii
Muktasari:
- Jumla ya timu 16 zitashiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026-2027 ikiwemo Kagera Sugar na Geita Gold zilizopanda daraja kutoka Ligi ya Championship.
Dar es Salaam. Wakati Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025-2026 ikichezwa kwa siku 286 kuanzia Septemba 17, 2025 hadi Juni 30, 2026, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kwamba, msimu ujao wa 2026-2027, ligi hiyo itachezwa kwa siku 275.
Hayo yamezungumzwa na Rais wa TFF, Wallace Karia wakati wa uzinduzi wa mfumo wa kidigitali wa kusimamia Ligi Kuu uliofanyika leo Alhamisi jijini Dar es Salaam.
Karia ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, amesema msimu wa 2026-2027 utafunguliwa kwa mechi ya Ngao ya Jamii itakayoikutanisha Yanga dhidi ya Simba ikipangwa kuchezwa Agosti 12, 2026, kisha ligi itaanza Agosti 14, 2026 hadi Mei 16, 2027.
"Mfumo wa Ngao ya Jamii kuwa na timu nne haujabadilika lakini kutokana na hili tulilonalo la uwenyeji wa AFCON 2027, tunalazimika kufanya mambo kwa haraka, hivyo tutakuwa na timu mbili tu, bingwa wa ligi ambaye ni Yanga na mshindi wa Kombe la CRDB, Simba. Mechi itachezwa Agosti 12.
"Ligi Kuu itaanza Agosti 14 na tunatarajia itamalizika Mei 16, 2027 ili kutoa nafasi kwa timu ya taifa kujiandaa na AFCON 2027," amesema Karia.
Kuhusu mfumo wa kidigitali wa kusimamia Ligi Kuu, Karia amesema utasaidia kupunguza malalamiko kwa waamuzi sambamba na ratiba.
"Mfumo huu utasaidia mambo mengi ikiwemo malalamiko ya klabu na viongozi kwa waamuzi, lakini pia wale wanaosema ratiba ni ngumu wachezaji wanacheza mechi mfululizo wanachoka.
"Ukiangalia tumetoa nafasi kwa timu kusajili wachezaji 40, hivyo hakuna sababu ya kusema uchovu wa wachezaji, lakini mfumo huu utasaidia sana kupambana na changamoto hizo," amebainisha Karia.
Katika hatua nyingine, Karia amesisitiza kwamba, hawana budi kumaliza msimu mapema licha ya kwamba kutakuwa na mashindano mengi ikiwemo mechi za kufuzu AFCON, hivyo siku yoyote kuanzia leo ratiba ya ligi itatangazwa.
Jumla ya timu 16 zitashiriki Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026-2027 ikiwemo Kagera Sugar na Geita Gold zilizopanda daraja kutoka Ligi ya Championship.