Yanga yaezidi kulisogelea, Ruvu hoi...

YANGA imeendeleza ubabe wake kwa Ruvu Shooting baada ya usiku wa leo kuibuka na ushindi wa bao 1-0, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa.

Bao pekee na la ushindi kwa Yanga limepatikana dakika ya 33 baada ya beki wa Ruvu Mpoki Mwakinyuke kujifunga kutokana na kukosa maelewano mazuri na mwenzake Rolland Msonjo kwenye harakati za kuokoa shambulizi.


Zifuatozo ni baadhi ya dondoo za timu hizo mbili;

Mechi tano za nyuma zilipokutana timu hizo kabla ya leo, Yanga ilishinda nne na moja kumalizika kwa suluhu (0-0)

Katika mechi zote hizo Yanga ilizoshinda iliruhusu walau bao moja hivyo haikuondoka uwanjani na ‘clean sheets’.

Mchezo wa leo ni wa nane mfululizo kwa Yanga kushinda kwenye ligi baada ya kupoteza kwa kuchapwa 2-1 na Ihefu Novemba 29, mwaka jana.

Mechi ya leo ni ya  16 mfululizo kwa Ruvu bila kupata ushindi kwenye ligi, mara ya mwisho kwa maafande hao kushinda ilikuwa Septemba 19 mwaka jana wakiichapa Coastal Union 2-1.

Ni mchezo wa sita mfululizo kwa Ruvu bila kupata bao lolote kwenye Ligi Kuu kwani mara ya mwisho kutikisa nyavu za mpinzani ilikuwa  Disemba 3, mwaka jana ikichapwa 2-1 na Dodoma Jiji.

Yanga imeendeleza rekodi yake ya kufunga bao kwenye kila mechi ya ligi kwa msimu huu, ikifikisha mabao 39.

Ushindi huo umewafanya Wanajangwani, Yanga kufikisha alama 53 na kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi, pointi sita zaidi ya Simba inayofuata ikiwa nazo 47 nafasi ya pili.

Ruvu  imeendelea kuburuza mkia na pointi zake 14 ilizovuna kwenye mechi 21, ikishinda tatu tu, sare tano na kupoteza 13.

Ruvu imesalia kuwa kundi moja na Simba ambazo ni timu pekee hazijafungwa na staa wa Yanga Fiston Mayele kwenye Ligi hadi sasa