Yanga yaizidi kete Rivers United

YANGA tayari ipo Uyo, Kusini mwa Nigeria kukiwasha na wenyeji Rivers United leo Jumapili. Lakini River wamezidiwa kete na Yanga na kujikuta wakikuna kichwa jinsi ya kuwakabili ndani na nje ya Uwanja.
Mpango wao wa kuchezea kwenye uwanja wao umekwama na wametupwa Uyo, Mastaa wao wawili wa Liberia hawatacheza dhidi ya Yanga.
Lakini Kocha wao anakuna kichwa jinsi ya kupambana na mastraika wa Yanga huku staa wake anayeongoza kwa mabao, raia wa Ghana akiwa hana uhakika wa kuikabili Yanga.
Ni hivi; Rivers walitaka mchezo huo wa robofainali uchezwe kwenye Uwanja wao wa Adokiye Amiesimaka Stadium ulioko Port Harcourt lakini Caf ikawagomea na kuamuru kipigwe Godswill Akpabio ulioko Uyo ambao wanaona ni kama ugenini.
Caf imeukaugua uwanja wao na hawakuridhika na matengenezo yake hivyo wakawaamuru waendelee kuufanyia ukarabati kwa hatua ijayo. Jambo hilo limewakera Rivers ambao walitaka kutumia faida ya mashabiki wao ambao huongozwa na matarumbeta.
Mechi hiyo itaanza saa 10 jioni, mwamuzi ni Abongile Tom wa Afrika Kusini.


WALIBERIA, MGHANA
Mastaa wao wa kutumainiwa kutoka Liberia, Albert Korvah na Mark Theo Gibson wataikosa mechi ya Yanga kwavile walishaichezea Watanga FC ya nchini kwao msimu huu.
Walijiunga na Rivers kwenye dirisha dogo kuongeza nguvu kwenye ushambuliaji na kiungo huku Kocha wao akiwataja kama wachezaji muhimu zaidi kwasasa kikosini lakini hawana namna zaidi ya kutii matakwa ya kanuni.
Kuhusu Mghana wao, Paul Acquah anayeongoza msimamo wa wafungaji wa shirikisho akiwa na mabao matano alikuwa majeruhi na ameanza mazoezi mepesi hivyo uwezekano wa kuikabili Yanga kesho bado ni finyu.
Kiungo huyo aliumia kwenye mechi ya makundi dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.


MASTAA WA YANGA
Kocha wa Rivers United, Stanley Eguma amesema kuwa timu yake italazimika kutumia staili tofauti kuikabili Yanga kwavile ni timu ngumu kwa mujibu wa dondoo alizonazo haswa kwenye ushambuliaji na inaongoza ligi huku .
Alisema hawatategemea historia ya misimu iliyopita kwenye mechi hizi mbili; "Yanga imetengeneza timu mpya kabisa tofauti na ile tuliyoitoa wakati ule."
"Najua pia wanaongoza Ligi kwao na walimaliza kundi wakiwa kileleni,"alisema Kocha huyo ambaye asilimia kubwa ya wachezaji pia ni wapya lengo likiwa ni kutinga nusu fainali kwa mara ya kwanza kwenye historia yao kama ilivyo kwa Yanga.