Yanga yanyemelea ubingwa, Guede akitupia

Bao la dakika ya 76 la Joseph Guede dhidi ya Coastal Union leo kwenye Uwanja wa Azam Complex, limeifanya Yanga kuzidi kujikita kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikifikisha pointi 61 na hivyo kuifanya ihitaji pointi 13 tu katika mechi sita ilizobakiza ili ijihakikishie ubingwa.

Guede alifunga bao hilo kwa shuti kali la mguu wa kulia akiunganisha mpira ulioshindwa kuokolewa na mabeki wa Coastal Union ambao ulitokea kwa beki wa kulia wa Yanga, Yao Attohoula.

Yanga ni kama ilitumia faida ya Coastal Union kuwa pungufu uwanjani kufuatia beki wake wa kati Lameck Lawi kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na refa Rafael Ikambi wa Morogoro baada ya kumchezea rafu, Stephane Aziz Ki aliyekuwa anaelekea kufunga.

Kadi hiyo hiyo aliyoonyeshwa Lawi, ni ya 17 kuonyeshwa katika Ligi Kuu msimu huu na anakuwa mchezaji wa pili wa Coastal Union kuonyeshwa kadi nyekundu msimu huu baada ya Hija Ugando ambaye alipata katika mechi dhidi ya Simba, Septemba 21 mwaka jana.

Yanga imeendeleza rekodi nzuri katika Ligi Kuu Bara mbele ya Coastal Union kwani tangu mara ya mwisho ilipofungwa mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga Machi 4, 2021 haijawahi kupoteza tena wala kutoka sare.

Mabao ya Coastal Union iliyokuwa chini ya Kocha Mkuu, Juma Mgunda yalifungwa na Erick Msagati na Mudathir Said huku lile la Yanga iliyokuwa inafundishwa na Kocha Mrundi, Cedric Kaze likifungwa na aliyekuwa nyota wa kikosi hicho Mkongomani, Tuisila Kisinda.

Tangu hapo Yanga ilipopoteza mchezo huo, imekutana na Coastal Union katika michezo sita ya Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hiyo imeshinda yote na kufunga jumla ya mabao 12 huku kwa upande wa Coastal ikiwa haijashinda wala kufunga bao lolote.

Mchezo wao wa kwanza kukutana msimu huu, Yanga ilishinda pia bao 1-0, lililofungwa na nyota wa timu hiyo, Clement Mzize dakika ya 71, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga Novemba 8, mwaka jana.

Huu ni mchezo wa pili kwa timu hizi kukutana Aprili tangu mwaka 2011 katika Ligi Kuu Bara ambapo mechi ya kwanza ilipigwa Aprili 8, 2015 na Yanga kuibuka na ushindi mnono wa mabao 8-0, ikiwa ni mechi iliyozalisha mabao mengi kwao tangu zilipoanza kukutana baina yao.

Katika michezo 24 Coastal Union iliyocheza msimu huu, imeshinda tisa, sare sita na kupoteza tisa ikiendelea kusalia nafasi ya nne na pointi 33.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema kuwa wangeweza kupata ushindi wa idadi kubwa ya mabao lakini uwezo wa kipa wa Coastal Union, Ray Matampi uliwanyima mabao.

"Kipa wao alikuwa bora sana kwani alifanya kazi ya kipekee kuokoa hatari nyingi. Tunapaswa kumpongeza pia na kocha wao alikuja na mpango bora lakini mwisho wa siku jambo la muhimu ni tumepata pointi tatu," alisema Gamondi.

Kocha wa Coastal Union, David Ouma alisema kuwa kadi nyekundu ambayo beki wake Lameck Lawi alipata katika dakika ya 70 iliwaathiri kwa kiasi kikubwa.


"Tukiwa 11 kwa 11 hawakuweza kufunga bao wakafanya hivyo baada ya sisi kubaki 10 hivyo nawapongeza wachezaji wangu kwa kucheza vizuri," alisema Ouma.