Yanga yatoa kauli kisa Lassine Kouma
Muktasari:
- Yanga msimu ujao itakuwa na kibarua cha kutetea makombe ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho la CRDB na Ngao ya Jamii.
Dar es Salaam. Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe ametamba kuwa mashabiki wa timu hiyo wajiandae kuona maajabu ya kiungo wao mpya Lassine Kouma.
Kouma amesajiliwa na Yanga hivi karibuni akitokea klabu ya Stade Malien ya Mali na Kamwe amesema watu wakae mkao wa kula kupata uhondo wa kiungo huyo mshambuliaji.
Anaitwa Lassine Kouma au sisi tumempa jina la KO Magic ni kijana wa maajabu kiukweli. Unajua uzuri mwaka huu sisi kama klabu tumeamua kukifanya, tusiingie kwenye huu ulimbukeni wa kujaza sana sifa wachezaji.
“Sisi tunaamini mafanikio ya taasisi yapo katika eneo la kuchezea hayapo Instagram. Sisi tunafukuzia mafanikio ya eneo la kuchezea. Tunasajili wachezaji, tunawaweka wapate muda mzuri wa kujiandaa kwa ajili ya kuisaidia timu,” amesema Kamwe.
Kamwe ameongeza kwamba wanahitaji kuona wachezaji wao wanapata sifa kwa kuonyesha kiwango bora na sio kupata sifa ambazo hawazitolei jasho.
Kamwe amesema kwamba kesho, Julai 27, 2025 wataendelea kutambulisha nyota wao wapya.
“Usajili unaendelea. Leo ilikuwa tuangushe vyuma vingine. Tumesimamisha hili zoezi la kuangusha vyuma leo, kesho utaratibu uko palepale.
“Uzuri Yanga huwa hatujaribu, wachezaji ni wetu, tumesajili wachezaji hatujasajili bangi kwa hiyo hatuna haja ya kumficha mtu. Kesho tunaangusha wachezaji wengine ambao tumesajili,” amesema Kamwe
Hadi sasa, Yanga imeshatangaza kusajili wachezaji wanne ambapo wawili ni wa kigeni na wengine wawili wazawa.
Wachezaji ambao Yanga imewasajili ni Lassine Kouma, Balla Conte, Offen Chikola na Abdulnasir Casemiro.
Wakati ikitambulisha wachezaji hao, Yanga imetangaza kuachana na wachezaji watano ambao ni Kennedy Musonda, Clatous Chama, Jonas Mkude, Khalid Aucho na Stephane Aziz.