Zahera atoa siri 7 za Ibenge, apania kuivusha Yanga kibabe

KOCHA wa zamani Yanga, Mwinyi Zahera ameipa timu hiyo siri saba za kumbwaga swahiba yake mkubwa, Florent Ibenge atakapokuja nchini na Al Hilal yake katika mechi ya kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wikiendi ijayo. Ibenge alikuwa na Zahera kwenye timu ya Taifa ya DR Congo kwa muda mrefu na habari zinasema pia wana makazi eneo moja nchini Ufaransa.

Zahera akizungumza na Mwanaspoti jana kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi Jijini Dar es Salaam majira ya Swala ya Ijumaa, alisema anafanya kazi kwa karibu sana na Kocha Mohammed Nabi na hata mechi hii wataicheza pamoja kimbinu. Ibenge yupo DR Congo kwa mechi ya kirafiki na TP Mazembe. Lakini akataja siri saba; Kwanza wachezaji wanatakiwa kuwa na kiu na hamu ya kuhitaji kufanya jambo kubwa katika mchezo huo hata wakikutana na changamoto ya aina yoyote ile hawatakiwi kurudi nyuma na kukata tamaa kwani Ibenge ni mjanja sana.

“Jambo la pili kila mchezaji atakayepata nafasi ya kucheza anatakiwa kujiamini na kutumiza majukumu yake yalivyo, kila mchezaji anatakiwa kupandisha ubora wake zaidi ya kawaida,” alisema Zahera na kuongezea;

“Wachezaji wa Yanga wote wanatakiwa kujitolea kwa asilimia mia ikitokea wakacheza kwa asilimia 70, maana yake hawataweza kushindana na wenzao kwani watakuja na ubora kuliko wao.”

“Jambo la tatu wachezaji wa Yanga wanatakiwa kuheshimu plani ya mchezo huo wakianzia katika uwanja wa mazoezi hadi muda wote wanapokuwa uwanjani kwenye mechi yenyewe kwani nafahamu watasoma na kuangalia video za Al Hilal vile ambavyo wanacheza.

“Katika kuangalia huko video wataona Al Hilal wachezaji wao wanashambuliaje na wanakaba kwa namna gani baada ya hapo wanatakiwa kuheshimu plani yao.”

Nondo ya nne aliyowapa ni kwamba wachezaji wa Yanga wanatakiwa kucheza zaidi kwa pamoja kwenye kushambulia na kukaba mashambulizi ya timu pinzani kwani si mechi ya uwezo wa mchezaji binafsi.

“Nimewaeleza hivyo kwa sababu Al Hilal kuna wachezaji wenye uwezo binafsi ambao anaweza kuwa mmoja dhidi ya watatu wa Yanga na akafanya jambo la hatari kwa maana hiyo kukaba kwa pamoja itakuwa na faida kwetu,” alisema Zahera na kuongeza;

“Cha tano; viongozi na wale wenye ushawishi kwenye timu si vyema kwenda kambini kuongea na wachezaji ikiwemo mambo ya kuwapa ahadi ya bonasi kwani inaweza kuwatoa mchezo na kuacha kufikiria kazi kubwa iliyokuwa mbele yao.

“Mechi kama hizi za Al Hilal hazihitaji maneno mengi kwani kila mchezaji mkubwa au yule mwenye wivu wa mafanikio anahitaji kujituma kwa nafasi yake ili kupata matokeo mazuri na hizo pesa kama bonasi zikaja kama sapraizi.

“Lakini lingine la sita; wale wazoefu kama Mayele, Bangala, Djuma aina ya mechi hizi ndio wanatakiwa kuonyesha ukubwa wao, kuitwa timu ya taifa kama watacheza kwa ubora.”

“Mwisho, Nabi anapafahamu Sudan alitoka kufundisha huko kabla ya kuja Yanga, wachezaji wa DR Congo waliyopo Yanga kumfahamu kwao kocha Ibenge kutakuwa na faida kwao ila wakifanya tofauti itakuwa shida sana.”