Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT-Wazalendo yasisitiza haki na usawa kwa Wazanzibari

Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman

Muktasari:

  • Othman Masoud Othman asema ACT-Wazalendo imejipanga kuinusuru Zanzibar kwa haki, ajira, heshima na usawa kwa kila mwananchi

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman amesema chama hicho kina mipango madhubuti ya kuendesha nchi kwa haki, heshima, ajira na maisha bora kwa kila mwananchi kulingana na rasilimali zilizopo.

Taarifa kwa vyombo vya habari ya ACT-Wazalendo iliyotolewa leo Juni 7, 2025, imeeleza kuwa, Othman ametoa kauli hiyo Julai 6, 2025 wakati akizungumza na wananchi, wanachama na wafuasi wa chama hicho katika Kisiwa cha Uzi Mkoa wa Kusini Unguja.

“Tunataka kurudisha heshima ya Taifa hili, ili uwe na haki na usawa kwa kila mmoja na watu wafaidike na matunda ya nchi yao na ndio maana tunasema huu ni mwaka wa kuinusuru Zanzibar,” amesema Othman.

Amesema mwananchi anapokuwa maskini ndivyo Taifa linavyokuwa maskini kwa sababu uimara wa uchumi wa nchi unaanzia kwa mwananchi wa kawaida.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema nchi hiyo ina mapato mengi lakini bila mamlaka kamili haiwezi kufikia huko, hivyo iwapo wakifanikiwa kushika madaraka wataondoa kodi ya mapato kwenye masuala ya Muungano.

Amesema hawatafikia mipango hiyo iwapo wananchi watafanya makosa kutokiweka madarakani chama hicho. “Tusifanye makosa mwaka huu, ACT tunadhamira ya kweli kuinusuru Zanzibar ili ifanye mambo yake yenyewe na iheshimiwe tofauti na ilivyo sasa.”

Othman amesema wakati Maalim Seif Sharif Hamad enzi za uhai wake aliingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa kutoa masharti matatu ya kutekelezwa, lakini yamekuwa yakisuasua na iwapo yangetekelezwa chama hicho kisingekuwa na la kusema kwa sasa.

Miongoni mwa masharti hayo ni kufanya uchunguzi na kubaini waliohusika na mauaji ya watu 21 katika uchaguzi wa mwaka 2020 na hatua zichukuliwe.

Pia, amesema kufanyike marekebisho ya sheria za uchaguzi kwa kuwa, ndio mzizi wa fitina katika nchi na iundwe tume ya maridhiano, lakini utekelezaji wake umekuwa changamoto.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Ismail Jussa amesema uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa aina yake na watakuja kuona kwenye sanduku la kura.

"Wazanzibari wote tuunganishe nguvu tuinusuru Zanzibar," amesema Jussa.

Pia, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar wa chama hicho, Omar Ali Shekhe amesema mara hii hawahitaji huruma ya mtu isipokuwa kura za wananchi ndio zitakipeleka chama hicho kushika dola.

Amesema mchakato wa chama kupata wagombea wa kupeperusha bendera zao kwa ngazi ya uwakilishi kwa majimbo 50 na wadi 111 tayari umekamilika. Mchakato huo ulianza Juni 18 hadi Julai 5, 2025.

"Mara hii ACT imedhamiria kuwaletea wagombea wazuri watakaoshinda kwa hiyo tuwapongeze wote waliotia nia kugombea,” amesema. 

Amesema Tume ya Uchaguzi ina dhamana ya kusimamia sekretarieti yake ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki na chama hicho hakipo tayari kuona unavurugwa, bali waache watu washindane wenyewe.

Katibu wa Ngome ya Vijana Taifa wa ACT Wazalendo, Muhamed Busara amewataka vijana wahamasishane kujitokeza kwa wingi kupiga kura wakati ukifika ili kuondoa utawala wa chama kilichopo madarakani.

"Tuhakikishe kila kijana anahamasisha makundi yote, tunahitaji hamasa kubwa kuelekea kwenye uchaguzi," amesema.

Naye Katibu wa Ngome ya Wanawake Mkoa wa Kati, Hidaya Yussuf Haji amesema wanawake ni nguvu kubwa, hivyo wasibaki nyuma kupiga kura na ikifika wahakikishe wanazilinda.

"Tusifanye masihara lazima tumpeleke OMO (Othman Masoud Othman) Ikulu,” amesema.

Amesema katika mkoa huo wanawake hawana kazi na wanaume wanajihusisha na uvuvi, lakini bado hawajanufaika nao kwa hiyo chama hicho ndio kina dhamira ya kuleta mabadiliko.

Kaimu Mwenyekiti Ngome ya Wazee Taifa, Masoud Khamis amesema hakuna wakati tena wa kuoneana haya na kuwataka wazee wasirudi nyuma kupambania mamlaka kamili ya Zanzibar.