Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Barrick-Twiga kinara wa gawio serikalini, yatoa Sh221.9 bilioni

Muktasari:

  • Katika hafla hiyo ya Gawio Day 2026, Rais Samia amepongeza taasisi na kampuni ambazo Serikali ina ubia nazo kwa kuendelea kufanya vizuri, akisema hatua hiyo inaongeza tija katika biashara na uwekezaji kwa manufaa ya Taifa.

Dar es Salaam. Serikali imepokea gawio la Sh221.9 bilioni kutoka ubia wa Kampuni ya Barrick Mining Corporation na Serikali kupitia Kampuni ya Twiga Minerals Corporation, huku kampuni hiyo ikiibuka kinara kwa kutoa gawio kubwa zaidi katika mwaka huu wa fedha.

Hundi ya mfano ya gawio hilo yenye thamani ya Sh221.9 bilioni imekabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, na Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dk Melkiory Ngido, katika hafla ya kupokea gawio na michango kutoka taasisi na mashirika mbalimbali ya umma iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo ya Gawio Day 2026, Rais Samia amepongeza taasisi na kampuni ambazo Serikali ina ubia nazo kwa kuendelea kufanya vizuri, akisema hatua hiyo inaongeza tija katika biashara na uwekezaji kwa manufaa ya Taifa.

Barrick-Twiga imeendelea kuongeza mchango wake kwa Serikali tangu kuanzishwa kwa ubia huo mwaka 2019. Katika mwaka wa fedha uliopita kampuni hiyo ilitoa gawio la Sh93.6 bilioni, huku mwaka 2022/23 ikitoa Sh84 bilioni na kushika nafasi ya kwanza, baada ya mwaka uliotangulia kutoa Sh53.5 bilioni.

Migodi inayosimamiwa na Barrick-Twiga nchini ni North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi ambao kwa sasa uko katika hatua za kufungwa na kubadilishwa kuwa eneo maalumu la uwekezaji wa kimataifa katika sekta ya madini linalojulikana kama Buzwagi Economic Special Zone.

Akizungumzia mafanikio hayo, Dk Ngido amesema mchango wa Barrick-Twiga hauishii kwenye gawio pekee bali kampuni hiyo imeendelea kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi, tozo mbalimbali, mishahara na malipo kwa wazabuni wa ndani.

Amesema uwekezaji wa kampuni hiyo umeendelea kuwanufaisha wananchi wanaozunguka migodi kupitia miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR), ikiwemo sekta za elimu, afya, maji safi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

“Mbali na kuchangia pato la Taifa, tunaendelea kuhakikisha jamii zinazozunguka migodi inanufaika kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema.

Dk Ngido ameongeza kuwa shughuli za Barrick nchini pia zimekuwa kichocheo cha ukuaji wa biashara za ndani kwa kuwapa fursa wazabuni na wakandarasi wazawa, pamoja na kuongeza ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Kwa upande wake, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema Gawio Day ni sehemu muhimu ya kujitathmini katika juhudi za mageuzi ya kiuchumi na kimkakati ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2020-2050.

Awali, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alisema tukio hilo lina umuhimu mkubwa kutokana na mchango wa gawio na hisa katika kukuza uchumi na uwekezaji wa Taifa.

Alisema mashirika ya umma na kampuni mbalimbali nchini zina nafasi kubwa katika kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi na kuongeza mapato kwenye mfuko mkuu wa Serikali.