Dk Nchimbi: Sitawaangusha Watanzania, mpigieni kura za kishindo Samia Oktoba 29
Muktasari:
- Dk Nchimbi yupo mkoani Ruvuma kuendelea na kampeni za CCM, ambapo amekuwa akihimiza wananchi kuendeleza amani, umoja na mshikamano huku akisisitiza umuhimu wa kufanya maamuzi ya busara katika uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.
Songea. Mgombea mwenza wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, amewaahidi wananchi wa Ruvuma na Watanzania kwa ujumla kuwa hatawaangusha endapo watakiamini chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Dk Nchimbi amewataka wananchi kumpigia kura za kishindo mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea wa ubunge na udiwani wa CCM, akisisitiza kuwa kufanya hivyo kutawawezesha viongozi hao kufanya kazi kwa umoja, bila vikwazo na kuharakisha maendeleo ya nchi.
Akizungumza leo Jumapili Oktoba 19, 2025 katika Uwanja wa Ndege wa Songea, akopokelewa na mamia ya wakazi wa mkoa huo, Dk Nchimbi amewataka wananchi wa Ruvuma kuitunza heshima na imani ambayo Rais Samia amewapa, kwa kumpa kura nyingi za ushindi ili aendelee kuwaletea maendeleo.
“Naomba msiniangushe. Tupigie kura nyingi kwa Mheshimiwa Mgombea wetu wa Urais, Samia, wabunge wote na madiwani wa CCM. Wote waongoze kwa kupata kura za kishindo ili nipate nguvu ya kujadili maendeleo bila woga,” amesema Dk Nchimbi.
Amesema atahakikisha anamsaidia Rais Samia katika juhudi za kuijenga nchi, akisisitiza kuwa serikali itakayoongozwa na CCM itaendelea kuzalisha fursa za kiuchumi, kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha miundombinu ya maendeleo.
Awali, mmoja wa wananchi waliojitokeza kumpokea aliyejitambulisha kwa jina la Diana Abdul alisema wana imani kubwa na Dk Nchimbi pamoja na mgombe urais, Samia kwamba wataendelea kuboresha maisha ya Watanzania, hususan wakulima wa Ruvuma.
“Nina imani kubwa na mgombea mwenza wetu pamoja na Samia. Wote ni wachapakazi na wapenzi wa watu. Tunaamini watahakikisha tunapata soko la uhakika la mazao yetu kama mahindi, mbaazi na korosho,” amesema Diana.
Naye Kudra Juma, mkazi wa Songea ametumia nafasi hiyo kumwomba Dk Nchimbi kuwasaidia wananchi wa Ruvuma kupata pembejeo za ruzuku kwa wakati na kwa bei nafuu, ili kuongeza tija katika kilimo.
“Tunamwomba mgombea mwenza atusaidie wakulima tupate pembejeo kwa bei nafuu na kwa wakati. Hilo litatusaidia sana kuongeza uzalishaji na kipato chetu,” amesema Kudra.