Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Faini, uchovu na ubovu wa barabara tishio kwa madereva

Kutoka Idara ya Usalama na Mazingira, Wizara ya Uchukuzi Marwa Chacha

Muktasari:

  • Madereva wa mabasi wamesema faini zisizotabirika, uchovu, ubovu wa barabara, foleni na maslahi madogo vinachangia msongo wa mawazo unaohatarisha afya ya akili na kuongeza ajali. Serikali na wadau wanasema zinaendelea kuchukulia hatua na kuboresha mazingira na usalama wa kazi.

Dar es Salaam. Faini zisizotabirika, uchovu unaotokana na safari ndefu, ubovu wa barabara, foleni na maslahi madogo ni miongoni mwa changamoto ambazo madereva wa mabasi na magari ya masafa marefu zimetajwa kuwa sababu zinazochangia changamoto ya afya yao ya akili kwa kuongeza hatari ya ajali zinazoweza kuzuilika.

Licha ya kutambua wajibu wao wa kuzingatia sheria za usalama barabarani, mazingira wanayofanyia kazi yamekuwa yakisababisha msongo wa mawazo unaowaathiri wanapokuwa barabarani.

Hayo yamesemwa Leo Jumanne Juni 30, 2026 na madereva wa gari la Isamilo la Dar es Salaam hadi Mwanza, Mayunga Julius walipokuwa wakipatiwa elimu ya afya ya akili katika mafunzo yaliyowakutanisha zaidi ya madereva 500, wakiwemo wanaofanya safari za ndani na nje ya nchi kupitia Kituo cha Kimataifa cha Mabasi cha Magufuli.

“Wakati mwingine tunatozwa faini ambayo hatukutarajia  huku nikiwa nimeendesha kwa saa nyingi bila kupumzika kutokana na ratiba za safari, hali ambayo huchosha akili na mwili na inaweza kusababisha makosa yanayoweza kuzuilika,”amesema Julius.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Wateja Latra Agustine Fungo.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Wateja  Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Agustine Fungo amesema sehemu ya faini wanazopata madereva zinatokana na kutofuata sheria na kanuni za usafirishaji, ikiwemo kubeba abiria zaidi ya idadi iliyoruhusiwa.

“Wengi wamekuwa wakiangukia katika faini kufuatia kushindwa kuzingatia sheria ikiwemo ya kubeba abiria kupita kiasi,”amesema Fungo.

Ofisa Elimu Msaidizi wa Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi (COTWU),Nice Amon amesema afya ya akili ya madereva ni sehemu muhimu ya usalama wa usafiri kwa kuwa wao hubeba maisha ya mamia ya abiria kila siku.

“Ndiyo maana chama hiki kwa kushirikiana na wadau wengine kimeanza kutoa elimu kwa madereva ili kuwasaidia kutambua dalili za msongo wa mawazo na namna ya kukabiliana nazo,”amesema Amon.

Kutoka Idara ya Usalama na Mazingir, Wizara ya Uchukuzi, Marwa Chacha amesema Serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto zinazowakabili madereva, ikiwemo kuandaa kanuni za uchovu wa madereva ili kuhakikisha wanapata muda wa kupumzika na kupunguza ajali zinazotokana na uchovu.

Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), James Richard amesema waajiri wana wajibu wa kuhakikisha madereva wanapata stahiki zao kwa wakati na kufanya kazi katika mazingira bora yatakayopunguza msongo wa mawazo.