Floton Africa yatoa Sh30 milioni kusaidia uanzishwaji kituo cha matibabu bingwa Tanzania
Muktasari:
- Floton Africa, ambayo ina uwekezaji katika eneo la Paje, Zanzibar, ilisema mchango huo ni sehemu ya mpango wake mpana wa uwajibikaji kwa jamii unaolenga kusaidia sekta mbalimbali ikiwamo afya, elimu, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii.
Unguja. Kampuni ya Floton Africa imetoa msaada wa Sh30 milioni kwa ajili ya kusaidia uanzishwaji wa Kituo Maalumu cha Upandikizaji wa Uboho na Matibabu katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya uchangishaji fedha inayolenga kupanua upatikanaji wa huduma za matibabu bingwa nchini Tanzania.
Msaada huo ulikabidhiwa Jumatano na Mkurugenzi wa Floton Africa, Swapna Brahmaroutu, kwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, katika hafla iliyowakutanisha viongozi wa Serikali pamoja na wadau mbalimbali.
Fedha hizo zitatumika kuunga mkono jitihada za kuanzisha huduma maalumu za matibabu kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za upandikizaji wa uboho, huku pia zikichangia katika juhudi za kitaifa za kuboresha huduma kwa wagonjwa wa selimundu pamoja na wale wanaohitaji huduma za upandikizaji wa figo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano, Mkurugenzi wa Floton Africa, Swapna Brahmaroutu, alisema mchango huo ni sehemu ya dhamira ya kampuni hiyo ya kuwekeza kwa jamii sambamba na kuchangia maendeleo ya miundombinu nchini.
“Katika Floton Africa tunaamini kuwa maendeleo endelevu hayaishii kwenye ujenzi wa majengo na miundombinu pekee. Yanahusisha pia kuwekeza kwa watu, kuimarisha huduma za afya na kujenga jamii zenye afya bora,” alisema.
Alisema kampuni hiyo inajivunia kuwa sehemu ya mpango huo muhimu wa afya, huku ikiamini kuwa mchango wake utasaidia kuleta matumaini mapya na kuboresha huduma za matibabu kwa familia nyingi nchini.
“Tuna matumaini kuwa mchango wetu utaleta matumaini na kuboresha huduma za afya kwa familia nyingi,” alisema.
Kampeni hiyo ya uchangishaji fedha ilizinduliwa wakati Hospitali ya Benjamin Mkapa ikiadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa na lengo la kuongeza uwezo wa kutoa huduma za matibabu bingwa ambazo awali hazikupatikana nchini na kuwasaidia wananchi kupata matibabu ndani ya Tanzania.
Baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, alisema kampeni hiyo inaratibiwa kitaifa na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), huku viongozi wa Serikali ngazi ya mikoa na wilaya wakihamasisha wananchi pamoja na wadau kuchangia.
Alisema huduma za matibabu bingwa zinazotolewa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa zimekuwa na umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar, kwani zimepunguza changamoto ya wagonjwa kusafiri kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu.
“Tunawahamasisha watu binafsi, kampuni na wawekezaji kuchangia katika jambo hili muhimu. Tunawashukuru Floton Africa kwa kuungana nasi kwa kutoa Sh30 milioni na tunatoa wito kwa wawekezaji wengine katika mkoa wetu kujitokeza kuunga mkono kampeni hii,” alisema.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kampeni hiyo ya uchangishaji fedha itaendelea hadi Julai 11, ambapo kutafanyika hafla ya kitaifa ya kuchangisha fedha jijini Dodoma.
Floton Africa, ambayo ina uwekezaji katika eneo la Paje, Zanzibar, ilisema mchango huo ni sehemu ya mpango wake mpana wa uwajibikaji kwa jamii unaolenga kusaidia sekta mbalimbali ikiwamo afya, elimu, uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii.
Kampuni hiyo ilieleza kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine katika kutekeleza miradi yenye manufaa ya muda mrefu kwa jamii na inayochangia maendeleo endelevu ya Tanzania.