Jaji Mkuu ahimiza OSHA kuendelea kukagua usalama maeneo ya kazi
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, George Masaju akifungua Mafunzo ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi yanayotolewa kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Muktasari:
- Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema Mahakama ni mdau muhimu katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.
Dodoma. Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Masaju, ameshauri Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuendelea kufanya ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini yakiwemo majengo ya Mahakama kwa mujibu wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Sura Na. 297, Marejeo ya 2023.
Ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo ya usalama na afya kazini ya siku mbili (Julai 2-3, 2026) yanayotolewa na OSHA kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani na Viongozi Waandamizi wa Mahakama.
Lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa viongozi hao wa Mhimili wa Mahakama ambao baadhi yao wameteuliwa hivi karibuni ili watekeleze majukumu yao ya msingi kwa kuzingatia viwango stahiki vya usalama na afya kwa mustakabali mzima wa afya, usalama, ustawi na maendeleo ya Taifa.
Jaji Mkuu amesema msingi wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan Ibara ya 12 na 14 zinazosisitiza juu ya umuhimu wa kulinda haki na utu wa watu.
“Kazi tunazozifanya hazipaswa kuhatarisha maisha yetu kwa namna yoyote ile na kimsingi tunafanya kazi kwa lengo ya kujiletea maendeleo ambayo kimantiki yanapangwa nasisi wenyewe ili yatusaidie sisi wenyewe hivyo ili kufaidi matunda ya maendeleo tunayoyatafuta hatuna budi kulinda afya zetu,” ameeleza Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, George Masaju akimpatia zawadi ya saa Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda baada ya hafla ufunguzi wa Mafunzo ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) yanayotolewa kwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania
Aidha, ameeleza mafunzo mbalimbali yakiwemo yanayohusu usalama na afya kazini ni muhimu kwa watumishi wa Mahakama na makundi mengine katika jamii kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa 2050 katika nguzo ya pili inayosisitiza juu ya uhitaji wa kujenga uwezo wa watu na jamii unaojumuisha ujuzi, stadi za maisha, uhuru wa kuchagua na kufanya maamuzi, pamoja na fursa zilizopo zinazomwezesha kila mtu kuishi maisha bora.
“Ili tuweze kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuimarisha mfumo wa utoaji haki na utawala bora nchini ni lazima tuhakikishe kwamba rasimali watu ya Mahakama inalindwa kupitia uboreshaji wa mazingira, miundombinu na kuiwezesha kupitia mafunzo kama haya,” amesema.
Akitoa salamu za awali katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema Mahakama ni mdau muhimu katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.
Amesema ni muhimu kuhakikisha kwamba kunakuwa na uelewa wa pamoja juu ya usimamizi masuala ya usalama na afya nchini baina ya OSHA na watendaji na viongozi wa Mahakama.
Amesema Taasisi ya OSHA itaendelea kushirikiana na Mahakama kupitia programu za mafunzo na uchunguzi wa afya za watendaji na viongozi wa Mahakama katika ngazi mbalimbali pamoja na kuhakikisha kwamba miundombinu ya Mahakama inafanyiwa ukaguzi ili kuhakikisha kwamba inakidhi viwango stahiki vya usalama na afya mahali pa kazi.
OSHA imekuwa ikitoa mafunzo ya usalama na afya kwa watendaji na viongozi wa Mahakama katika ngazi mbalimbali kwa awamu tofauti ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa Taasisi wa kuyafikia makundi mbalimbali ya wadau.
Awamu hii inawahusu Majaji 24 wa Mahakama ya Rufani pamoja na Viongozi Waandamizi wa Mahakama ambao sambamba na kupatiwa mafunzo, wamekabidhiwa vifaa muhimu vikiwemo viti vya igonomia na masanduku ya huduma ya kwanza.